Dodoma
Serikali ya Tanzania na Marekani zimeendelea kuimarisha ushirikiano wa kikazi katika sekta ya madini, hususan kwenye utafiti wa kina wa madini ya kimkakati yakiwemo madini ya kinywe, kwa lengo la kuimarisha usimamizi, tija, ajira na mchango wa sekta hiyo katika pato la Taifa.
Akizungumza leo Januari 21, 2025 jijini Dodoma wakati wa kikao kilichohusisha ujumbe maalum kutoka Ubalozi wa Marekani ulioongozwa na Mhe. Andrew Lentz, Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini pamoja na wataalamu wa Wizara ya Madini, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema ushirikiano huo unatekelezwa kupitia Wizara ya Nishati na Madini ya Marekani (US Department of States Enegry and Mineral Governance Program) na unalenga kuinua uwezo wa kitaifa katika utafutaji wa madini (Mineral exploration) na usimamizi wa Sekta kwa ujumla.
Aidha, Waziri Mavunde kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, ameshukuru Serikali ya Marekani ambayo kwa miongo kadhaa sasa imekuwa mshirika mkubwa wa maendeleo ya Tanzania kupitia misaada mbalimbali ya kiufundi na kifedha, Mhe. Waziri amebanisha kuwa serikali ya Marekani imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania katika miradi mbalimbali inayohusu sekta za elimu, kilimo, miundombinu, afya, masuala ya utawala bora na demokrasia na mengine mengi.
Waziri Mavunde amesema kuwa misaada ya kiufundi inayotolewa na Serikali ya Marekani, ikiwemo vitendea kazi kama vishikwambi na zana nyingine za kisasa za ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za jiosayansi, ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya Serikali ya Marekani ya kuimarisha usimamizi wa Sekta ya Madini na hivyo kuunga mkono ajenda muhimu ya maendeleo ya nchi yetu.
Ameeleza kuwa ni wakati muafaka kwa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kutumia fursa hiyo kikamilifu kwa kuongeza ujuzi na uwezo katika ukusanyaji, utunzaji, uchakataji na usambazajiwa taarifa za utafiti wa jiosayansi (Geo-data) kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Aidha, Waziri Mavunde amesema ushirikiano huo wa kuimarisha shughuli za utafiti za pamoja unatarajiwa kusaidia kubaini na kuibua migodi mikubwa ya madini ya kinywe katika mikoa ya Mtwara na Lindi. Hatua hii itaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa madini ya kinywe duniani. Waziri Mavunde alibainisha kuwa ifikapo mwaka 2050, uhitaji wa madini ya kinywe duniani utakuwa takriban tani milioni 4.5. Hii inathibitisha uhitaji mkubwa wa madini hayo kulinganisha na hali halisi ya upatikanaji wake kwa sasa.
Vilevile, Waziri amesema kupitia ushirikiano huu wataalamu wetu wa GST na STAMICO, watapata mafunzo yatakayowajengea uwezo wa kuweza kufanya utafutaji madini kwa njia za kisasa zaidi (state of art technologies) na pia kuongeza weledi kwa ujumla katika masuala yote yanayohusu usimamizi na uendelezaji miradi ya madini.
Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Balozi Andrew Lentz, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano wa kikazi unaolenga matumizi ya teknolojia za kisasa, hususan katika sekta ya nishati safi na salama zitokanazo na vyanzo jadidifu, kuanzia madini ya kimkakati hadi yale muhimu kwa ajili ya maendeleo ya viwanda.
Balozi Lentz ameongeza kuwa msaada wa kiufundi unaotolewa katika eneo la utafutaji wa madini utaboresha kwa kiwango kikubwa matumizi ya mbinu nateknolojia za kisasa zaidi katika utafiti, usimamizi na uhifadhi wa taarifa a za jiosayansi, hivyo kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha tafiti za madini katika ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.










No comments:
Post a Comment