MAMLAKA ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Tanga imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara, ambapo asilimia 80 ya miradi ya mwaka wa fedha 2024/2025 tayari imekamilika.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Meneja wa TARURA mkoa wa Tanga, Mhandisi George Tarimo, amesema kuwa asilimia 20 iliyosalia ya miradi ipo katika hatua za mwisho na inatarajiwa kukamilika kwa mujibu wa ratiba zilizopangwa.
Mhandisi Tarimo amesema mafanikio hayo yametokana na usimamizi mzuri wa miradi pamoja na kuimarika kwa upatikanaji wa fedha, akibainisha kuwa katika miaka ya nyuma TARURA ilikuwa ikitegemea zaidi Mfuko wa Barabara (Road Fund) kama chanzo kikuu cha ufadhili.
Akizungumzia mwaka wa fedha wa sasa 2025/2026, Mhandisi Tarimo amesema TARURA tayari imeanza utekelezaji wa miradi mipya, ambapo miradi 28 imeshakabidhiwa rasmi kwa wakandarasi kwa ajili ya utekelezaji.
Ameongeza kuwa kwa ujumla, miradi 125 ya barabara inatarajiwa kutekelezwa katika mkoa wa Tanga ndani ya mwaka huu wa fedha, hali inayoonesha ongezeko kubwa la bajeti na wigo wa miradi ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita.
Kwa mujibu wa Mhandisi Tarimo, jumla ya shilingi bilioni 37.7 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara mkoani Tanga kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Amesema fedha hizo zimetokana na vyanzo vitatu vikuu ambavyo ni Shilingi bilioni 13.2 kutoka Mfuko wa Barabara (Road Fund), Shilingi bilioni 6.5 kutoka Fedha za Maendeleo ya Majimbo, Shilingi bilioni 7.4 kutoka tozo ya mafuta.
Pia Amesema kuongezeka na kutofautishwa kwa vyanzo vya fedha kumeimarisha uwezo wa TARURA kutekeleza miradi mingi kwa wakati mmoja na kupunguza utegemezi wa chanzo kimoja cha fedha.
Mhandisi Tarimo ameongeza kuwa TARURA inaendelea na ukarabati wa miundombinu ya barabara licha ya changamoto ya baadhi ya miundombinu hiyo kuharibiwa kwa makusudi na watu wenye nia ovu.
Ametaja taa za barabarani kuwa miongoni mwa maeneo yaliyokuwa yakichangia gharama kubwa za matumizi ya umeme, hali iliyosababisha TARURA kuanza kubadilisha taa za umeme wa kawaida na kuweka taa zinazotumia nishati ya jua (solar).
Zoezi hilo tayari limeanza katika baadhi ya maeneo na litaendelea sambamba na miradi ya sasa na ijayo ya ukarabati wa barabara katika mkoa huo.
Aidha, Mhandisi Tarimo aliendelea kusema TARURA inaendelea kutekeleza mkakati maalum unaoendana na sera ya umiliki wa asilimia 30 kwa wananchi, unaolenga kuwawezesha wakazi wa maeneo husika kushiriki kikamilifu katika matengenezo ya miundombinu ya barabara.
Mkakati huo unatekelezwa kupitia mpango wa Community-Based Routine Maintenance, unaowawezesha wananchi kufanya matengenezo madogo ya barabara na kulipwa kwa kazi hiyo.
Mpango huo unatarajiwa kuanza awali katika maeneo ya Korogwe, Lushoto na Pangani, ambako tayari kuna vikundi vya wananchi vilivyosajiliwa, na unalenga pia kuzalisha ajira na kuimarisha umiliki wa miundombinu kwa wananchi.
Mhandisi George Tarimo amewahimiza wananchi wa mkoa wa Tanga kulinda na kutunza miundombinu ya barabara, akisisitiza kuwa utunzaji wa rasilimali za umma ni nguzo muhimu katika kuharakisha maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi ya mkoa huo.




No comments:
Post a Comment