Wednesday, January 28, 2026

SERIKALI YAELEZA SABABU ZA KUTOWALAZIMISHA WATOTO KUWAHUDUMIA WAZAZI.



Na Jackline Minja MJJWM-Dodoma 

Serikali imesema haina haja ya kuweka sharti la kisheria linalowalazimisha watoto kuwahudumia wazazi wao wasiojiweza, ikieleza kuwa suala hilo tayari linashughulikiwa kupitia misingi ya kifamilia na kijamii.

Kauli hiyo imetolewa bungeni na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa kinondoni Mhe. Tarimba Gulam Abbas lililohoji "Je Serikali haioni haja ya kuweka sharti la kisheria la watoto wakubwa kutunza wazazi wao wasiojiweza"?

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Mahundi amesema Serikali inatambua umuhimu wa familia na jamii katika kuchukua jukumu la kulea na kuwahudumia wazee, akisisitiza kuwa huo ni msingi wa mila na desturi za Watanzania.

Aliongeza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha huduma na matunzo kwa wazee kupitia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003, Toleo la mwaka 2024, ambayo inasisitiza wajibu wa familia na jamii katika kuwahudumia wazee wao.

“Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa familia na jamii katika kuchukua jukumu la kulea na kutunza wazee, kwani huu ndio msingi wa mila na desturi za Kitanzania na nguzo muhimu katika kujenga mshikamano wa kijamii," amesema 

Amesema pia kuwa katika kuimarisha huduma na matunzo kwa wazee, Serikali imefanikiwa kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 na kuandaa toleo la mwaka 2024, ambalo linaeleza bayana wajibu wa familia na jamii katika kusimamia matunzo ya wazazi na wazee kwa ujumla, Sera hiyo pia imeweka msisitizo wa kuimarisha mifumo ya kisheria utakaolinda na kuendeleza ustawi wa wazee pamoja na watoto wanaowatunza. 

Amsema kuwa kwa sasa Serikali ipo katika hatua ya kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kutoa maoni juu ya masuala muhimu ya kuzingatiwa katika sheria hiyo.

Hata hivyo, amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuhamasisha maadili ya uwajibikaji wa kifamilia na kuimarisha mifumo ya kijamii inayosaidia ustawi wa wazee nchini.

No comments:

DKT. MWIGULU AKUTANA NA FREDERICK SUMAYE

  Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Januari 28, 2026 amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye ofisini kwa Waziri Mku...