Wednesday, January 28, 2026

MAMLAKA YA BIMA KANDA YA ZIWA YA KUTANA NA MAMENEJA

 





Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Kanda ya Ziwa imefanya kikaokazi na Mameneja wa Kampuni za Bima zinazofanya shughuli zake katika kanda hiyo, kwa lengo la kuweka mikakati madhubuti ya kufikia wananchi wengi zaidi na kuongeza mchango wa sekta ya bima katika pato ghafi la kanda ya Ziwa.

Kaimu Meneja TIRA Kanda ya Ziwa, Bw. Oyuke Phostine, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya Mamlaka na Kampuni za Bima ili kupanua wigo wa huduma za bima.

“Bado kuna idadi kubwa ya wananchi katika kanda ya ziwa ambao hawajafikiwa na huduma za bima, hivyo kunahitajika mikakati ya pamoja ya elimu kwa umma, ubunifu wa bidhaa na matumizi ya teknolojia rahisi kuwafikia wananchi wa kada zote” alisisitiza Bw. Oyuke.

Aidha, kikao hicho kimejadili mikakati ya kuongeza pato ghafi la bima katika kanda ya Ziwa kwa kuimarisha mauzo ya bidhaa za bima zinazokidhi mahitaji halisi ya wananchi, hususan katika sekta za afya, kilimo, madini, ufugaji, uvuvi, biashara ndogo ndogo na usafirishaji.

Bw. Oyuke amewahimiza Mameneja wa Kampuni za Bima kuhakikisha wanazingatia viwango vya kitaaluma, maadili ya kazi na ufanisi katika kuhudumia wateja, ili kujenga imani ya wananchi kwa sekta ya bima.

Kikao hicho kimehitimishwa kwa makubaliano ya kuendelea kufanya usajili wa mawakala na mbinu mpya za usambazaji bima ili kutekeleza kwa urahisi mikakati iliyopangwa na kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa manufaa ya wananchi na ukuaji wa sekta ya bima katika Kanda ya Ziwa.


No comments:

SERIKALI YATOA MIKOPO KIASI CHA SHILINGI MILIONI 600 KWA WANANCHI

Halmashauri ya Mji Ifakara Januari 27,2026 imetoa mikopo ya asilimia 10 yenye thamani ya Shilingi milioni 600 ikiwa ni Mikopo ya Asilimia 10...