Mhandisi Mzawa akimuelekeza jambo Mstahiki
Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita wakipolikuwa kwenye eneo la mradi.
NA CHRISTINA MWAGALA,(OMJ) , Dar es Salaam.
MEYA wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita
ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa kuhimili athari za mabadiliko ya
tabia nchi pamoja na maboresho ya maeneo ya umma katika fukwe ya Ocean
Road.
Mradi huo ambao unatarajiwa kumalizika Oktoba
mwaka huu, utakuwa ni mahususi kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam kwa ajili
kutunza mazingira na kuepukana na mafuriko.
Alifafanua kwamba, mradi huo utahusisha ujenzi
wa vyoo na mabenchi ya kupumzikia, utakuwa na jumla ya urefu wa mita 860
kuanzia Hospitali ya Agha-Khani kupitia viwanja vya Ikulu.
“Ukiangalia kwenye fukwe zetu hazina vyoo,
hivyo kuwafanya watu wanaokuja kupumzika kukosa sehemu za kwenda kujihifadhi,
jambo ambalo sio zuri, ukizingatia jiji letu linapokea wageni kutoka sehemu
mbalimbali, ndio maana tumeamua kuleta mradi huu ili kuondoa aibu hii”
alifafanua.
Katika ziara hiyo iliyofanyika hivi karibuni,
Meya alisema kwamba maeneo ya kupumzikia katika jiji la Dar es Salaam sio
rafiki kutokana na ukosefu wa miundombinu hivyo kukamilika kwa mradi huu
kutaondoa baadhi ya changamoto zilizopo kwenye maeneo ya hayo.
“Jiji letu ukiangalia kimiundombinu haliko
vizuri, mpangilio wake pia hauko vizuri, sasa inapotokea mabadiliko yoyote,
wananchi hujikuta kwenye athari kubwa sana, hivyo kupitia mradi huu, utaondoa
changamoto hizi” alisema Meya.
“ Ukienda kwenye majiji mengine, utakuta
sehemu za fukwe kama hizi , watu wanapumzika, lakini pia ni chanzo cha mapato
kwa jiji kwa sababu wanalipia, ila kwetu hapa, imekuwa ni jambo la kawaida,
watu wakuja kupumzika kiholela, huu ndio muda wetu wa kulibadilisha jiji letu
la Dar es Salaam” aliongeza.
Akizungumzia vikundi mbalimbali ambavyo
vilipewa mikopo kwa ajili ya kujiendeleza, Meya Isaya alisisitiza kwamba, bado
nafasi zipo kwa vikundi vingine vinavyohitaji mikopo kwa masharti ya uaminifu.
Alifafanua kwamba vikundi vyote ambavyo
vitakidhi vigezo, vitapewa mikopo na kwamba lengo kubwa ni kuwakwamua wananchi
kiuchumi kupitia vikundi ambavyo vimeamua kujitoa kwa ajili ya kupambana na
umasikini.
No comments:
Post a Comment