Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania Bi. Beatrice Singano kushoto pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank Bw. Ibrahim Mwangalaba wakisaini makubaliano baina ya kampuni hizo mbili katika uzinduzi wa huduma mpya ya Timiza Vikoba, jana jijini Dar es Salaam.
Maendeleo Bank kwa kushirikiana na Airtel Tanzania jana wamezindua huduma mpya ijulikanayo kama Timiza Vikoba yenye lengo la kuviwezesha vikundi vya vikoba nchini kutumia njia ya kisasa na salama itakayorahisisha ukusanyaji wa michango, kutoa mikopo na marejesho ya mikopo ya mikopo kwa urahisi kabisa.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania Bi. Beatrice Singano na Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank Bw. Ibrahim Mwangalaba wakibadilishana nyaraka baada ya kusaini makubaliano baina ya kampuni hizo mbili katika uzinduzi wa huduma mpya ya Timiza Vikoba.
Huduma hii ya Timiza Vikoba inawawezesha wateja wa Airtel na Maendeleo Bank walio katika vikundi vya kuanzia watu 5 hadi 50 kupata huduma za kifedha masaa 24 siku saba za wiki kwa gharama nafuu kwa kupiga *150*60# na kisha kuingia kwenye menu ya Airtel Money na kusajili kikundi na kufungua akaunti ili kufaidika na huduma ya kutuma michango yao ya kila wiki, kuomba mikopo na kufanya marejesho ya mikopo kwakiwa nyumbani au mahali popote pale kwa usalama na urahisi zaidi.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank, Ndugu Ibrahim Mwangalaba alisema “Maendeleo Bank ni benki inayokua kwa kasi nchini kwa kutoa huduma mbalimbali zenye gharama nafuu, zenye urahisi wa kutumia ikiwemo ile ya akaunti za kuweka akiba, kutoa mikopo na huduma nyingine nyingi”.
Maendeleo Bank leo tunajisikia fahari kushirikiana na Airtel katika kuleta huduma ya Timiza Vikoba, huduma hii itasaidia wajasiriamali wadogo na wa kati kuweza kuweka akiba kupitia simu zao za mikononi ili kufungua fursa mpya katika huduma za kifedha nchini.
“Dhamira yetu ni kuenedeleza tabia ya kujiwekea akiba katika jamii na pia kuwapa wateja uwezo wa kukopa na kupokea mikopo kupitia simu zao za mikononi kwa kuwa tunaamini ni ni njia bora na rahisi Zaidi kuliko ile iliyozoeleka. Mteja ukitumia huduma hii ya mikopo ya Timiza Vikoba unajitengenezea historia yako ya mkopo kidogo kidogo na baadae kujipatia mkopo mkubwa kwa masharti rahisi Zaidi”
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel, Bi Beatrice Singano Mallya alisema “huduma ya Airtel Money imekuwa ikiongoza kwa huduma za kibunifu na kisasa Zaidi na leo hii tunazindua ushirikiano wa kipekee na Maendeleo Bank kupitia huduma ya Timiza Vikoba ili kuwawezesha wafanyabiashara katika vikundi vya Vikoba nchi nzima kufanya miamala yao ya kifedha kwa njia salama, uhakika na urahisi zaidi.
Huduma hii italeta uwazi na kuviwezesha vikundi vya Vikoba kuhakiki taarifa zao kwa kwa kupata taarifa za miamala mbalimbali kwa wakati kupitia simu zao za mikononi. Tunaamini huduma hii itachochea wafanyabiashara bila kujali maeneo walioko kujiunga na kutengeneza vikundi vya Vikoba ili kunufaika na kukuza biashara zao.
No comments:
Post a Comment