Rais Kikwete anatarajia kuzindua Kituo Kituo cha Michezo cha Kisasa cha Jakaya M. Kikwete Youth Park (JMK Park), Kidongo Chekundu, Dar es Salaam, kituo cha kwanza cha aina yake nchini chenye kulenga miongoni mwa mambo mengi kuanza kulea wanamichezo tokea wakiwa wadogo.
Hayo yalijitokeza wakati wa mazungumzo kati ya Rais Kikwete na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Umeme ya Symbion Power, Bwana Paul Hinks(pichani) kwenye Hoteli ya JW Marriot Essex House, mjini New York, Marekani ambako Rais alikuwa anafanya ziara rasmi ya kikazi. Rais Kikwete alikiwekea Kituo hicho jiwe la msingi mwaka jana.
Katika mkutano huo, uliofanyika jana, Jumanne, Septemba 29, 2015, Bwana Hinks alimweleza Rais Kikwete kuwa ujenzi wa Kituo hicho sasa umekamilika tayari kwa uzinduzi na hivyo kuongeza thamani kubwa kwenye eneo ambalo miaka ya nyuma lilikuwa gereji ya kutengenezea magari.
Kituo hicho cha JMK Park kimegharimu kiasi cha dola za Marekani milioni mbili na ni matokeo ya ushirikiano ya Kampuni ya Symbion Power ya Marekani, Klabu ya Soka la Ligi Kuu ya Uingereza ya Sunderland AFC na Taasisi ya Grasshopper Soccer.
(Picha na Freddy Maro).
No comments:
Post a Comment