Friday, October 30, 2015

MAGUFULI AKABIDHIWA HATI YA USHINDI NAFASI YA URAIS

Rais mteule wa Tanzania John Pombe Magufuli akionesha cheti chake cha ushindi alichokabidhiwa muda huu katika ukumbi wa Diamond Jubilee



Na Anitha Jonas na Beatrice Lyimo- MAELEZO.
 
Watanzania wametakiwa kukubaliana na matokeo ya  Uchaguzi Mkuu  wa mwaka 2015, yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) kwa kuwa  ni ya haki na hakuna aliyeibiwa kura.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Waangalizi wa Uchaguzi kutoka nchi za Jumuiya ya Madola nchini na ambaye Rais Mstaafu wa Nigeria, Goodlucky Jonathan kwenye halfa ya kumkabidhi hati Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyofanyika  leo kwenye ukumbi wa Diamond  Jubilee  jijini Dar es salaam.

“Uchaguzi ulikuwa wa haki na amani na hakuna yeyote aliyeibiwa haki yake kwani matokeo hayo yamedhibitishwa kuwa ya uhuru na haki kwa kufuata misingi ya sheria na taratibu zilizopo” alisema  Rais Mstaafu Jonathan.

Kwa upande wa mgombea urais kupitia chama cha ACT wazalendo Bibi. Anna Mghwira amesema kuwa chama chake kimemkubali matokeo ya uchaguzi uliompitisha Dkt. John Magufuli.

Vilevile ameongeza kuwa wagombea wote walizungumza kuhusu mabadiliko hivyo ana imani na mshindi wa nafasi hii atalisimamia ipasavyo.

“Watanzania wanahitaji mabadiliko hasa katika Katiba Mpya itakayotokana na maoni ya Watanzania, kuimarisha umoja wa kimataifa, kuinua uchumi wa nchi, kusimamia shughuli za Serikali pamoja na kuboresha usawa wa kijinsia kati ya mwanamke na mwanamume,” aliongeza Bibi Mghwira.

Mbali na hayo mgombea huyo wa urais kupitia chama cha ACT wazalendo amemkabidhi Rais Mteule Ilani ya chama hicho kama muongozo kwa yale yaliyopungua katika Ilani ya cha chake.

Aidha Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) Jaji Mstaafu Damian Lubuva amewapongeza wananchi kwa kuwa na mwamko mkubwa wa kupiga kura na kuliendesha zoezi hilo kwa amani.

Pia Jaji Mstaafu Lubuva alimkabidhi hati ya ushindi mgombea Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...