Monday, June 30, 2014

HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUHITIMISHA MKUTANO WA KUMI NA TANO WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 28 JUNI, 2014

 Waziri Mkuu Mizengo Pinda
---
 HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUHITIMISHA MKUTANO WA KUMI NA TANO WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 28 JUNI, 2014
  UTANGULIZI


a)    Masuala ya Jumla

Mheshimiwa Spika, 1.    Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutupatia uzima na afya hadi kufikia siku ya leo. Tumekuwepo hapa kwa takriban miezi miwili ambapo tumeweza kupokea na kujadili Taarifa za Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2013/2014 na Mwelekeo kwa mwaka 2014/2015 kwa Wizara mbalimbali na hatimaye kupitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2014/2015. 


2.    Napenda kutumia nafasi hii ya awali kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kazi nzuri ya kutukuka ambayo wameifanya kwa nidhamu na ufanisi mkubwa, hususan wakati wa Mjadala wa Bajeti ya Serikali na Mafungu ya Wizara za Kisekta. Kipekee niwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Bajeti chini ya Uongozi mahiri wa Mheshimiwa Mtemi Andrew John Chenge, Mbunge wa Jimbo la Bariadi Magharibi kwa kazi yao nzuri ya kuchambua Bajeti ya Serikali na Sheria zinazoambatana na masuala ya Bajeti. Changamoto zilikuwa nyingi,   lakini   kwa   pamoja   tumekubaliana   na   kuafikiana. Kazi kubwa iliyoko mbele yetu ni kwenda kushirikiana na Wananchi katika utekelezaji wa Bajeti hii ili kuwaletea maendeleo.


Mheshimiwa Spika, 3.    Katika kipindi hiki tukiwa hapa Bungeni, yapo matukio ya kusikitisha yaliyotokea ambapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walipoteza Wapendwa wao. Aidha, yapo matukio ya Kitaifa yaliyosababisha kupoteza maisha ya Ndugu, Jamaa na Marafiki. Napenda kutumia nafasi hii kuwapa pole Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote waliofikwa na misiba na majanga mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wote waliopotelewa na Ndugu, Jamaa na Marafiki.



Mheshimiwa Spika, 4.    Kipekee niwape pole ndugu, jamaa na marafiki waliopotelewa na ndugu zao na wote waliopata majeraha wakati kulipotokea Mlipuko wa Bomu pale Darajani, Zanzibar. Tukio hili la kusikitisha halipendezi kwa Nchi yetu. Niwaombe Wananchi wote kwa umoja wetu tushirikiane kuwa Walinzi katika maeneo yetu na kuwezesha kuwatambua mapema wale wote wenye nia mbaya ya kuharibu amani na utulivu katika Taifa letu.

No comments: