Wednesday, April 03, 2013

NHC WASIKITISHWA KUPOROMOKA GHOROFA DAR

 Baadhi ya wanahabari wakiwaombea dua watu waliokufa na kujeruhiwa baada ya kuporomokewa na  jengo la ghorofa 16, Mtaa wa Indira Gandhi, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Nyumba (NHC), Nehemia Mchechu (katikati) akiwaongoza Mkurugenzi wa Usimamizi wa Miliki wa (NHC), Hamad Abdallah (kulia) pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa Jamii wa shirika hilo, Suzan Omari, kuwaombea dua watu wote waliokufa baada ya kuporomokewa na jengo la ghorofa 16, Mtaa wa Indira Gandhi, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Tukio hilo walilifanya katika mkutano na wanahabari wa kuelezea kuanguka kwa ghorofa hilo, Dar es Salaam leo..
 Wanahabari wakiwa kazini
 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Nyumba (NHC), Nehemia Mchechu akijibu maswali mbalimbali ya wanahabari
Na Said Mwishehe
MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu amesema amesikitishwa na kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu 34.
Pia ameweka wazi kuwa jengo hilo ujenzi wake haukuwa imara kwani hata kwa macho kinachoonekana ni kifusi cha mchanga na nondo mpya. Jengo hilo lilikuwa linamikiwa na Ladha Construction Company Limited likiwa kiwanja namba 2032/73 Mtaa wa Indira Gandhi na Morogoro.
Shirika hilo lilikuwa na ubia kati yao na Ladha ambapo wao wanahusika kwa kutoa kiwanja, lakini hawahusiki na aina yoyote ile ya ujenzi.
Akizungumza Dar es Salaam jana wakati akifafanua kuhusu ubia uliopo kati yao na Ladha Construction, alisema: ”Ukiniuliza jengo lile ubora wake ulikuaje kwangu mimi binafsi naweza kusema kilichokuwepo pale ni kifusi cha mchanga mweusi na nondo mpya.
”Ni kitu ambacho kimekera watu wengi na kwetu kama shirika tumeumia zaidi. Hata hivyo, hatuwezi kulizungumzia sana kwa kuwa tayari vyombo vya sheria vinaendelea na uchunguzi wake ili waliohusika kuchukuliwa hatua,”.
Akizungumzia zaidi kuhusu wajibu wa kimkataba kati ya NHC na mbia wa jengo hilo alisema ulisainiwa Februari 4, 2007 ambapo katika ubia huo shirika ilikuwa liwe na hisa ya asilimia 25 na mbia asilimia 75 mara baada ya mradi kukamilika.
“Shirika la nyumba lilitoa ardhi ambayo ilikuwa ikihesabiwa kama asilimia 25 ya mtaji  wake kwenye jengo husika na mbia alikuwa na asilimia 75 na alitakiwa kugharamia ujenzi wote pamoja na usimamizi wa ujenzi.
”NHC wangepata asilimia nyingine 25 baada ya miaka 12 na wabia wangebakiwa na asilimia 50 kwa maisha yote,” alisema.
“Hivyo Desemba 4, 2007 mbia alipata kibali cha ujenzi wa jengo husika kutoka Manispaa ya Ilala chenye namba BP 34259 kilichomruhusu kujenga ghorofa 10 tu.
”Pamoja na kuonesha utashi na kuingia mkataba wa NHC wa kujenga ghorofa 12 katika kiwanja husika, mwenye mamlaka ya mwisho ya kuidhinisha ujenzi unaotakiwa ni mamlaka za mipango miji baada ya kuzingatia mpango wa endelezaji ulioko katika eneo husika.
“Makubaliano ya mkataba wa ubia kati ya NHC na mbia yanaonesha kazi ya mbia ni kugharimia ujenzi wote na NHC ilikuwa na wajibu wa kutoa ardhi ya kujenga ambayo ni hicho kiwanja.
”Tunaamini wataalamu aliowatafuta na kupata vibali vya mamlaka husika vya kuwatumia kujenga jengo hilo wanaaminika na mamlaka zenye dhamana ya  kuthibitisha sifa zao,” alisema.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...