Monday, August 08, 2011

Suala la mafuta bado shida kubwa

Foleni katika kituo cha mafuta GBP Sinza. Picha zote za Jackson Odoyo.


Wamiliki wa vituo mbalimbali vya mafuta jijini Dar es Salaam wamepuuza onyo la serikali la kushusha bei ya mafuta baada ya kuendelea na mgomo.

Vurugu katika soko la mafuta zilianza Agosti 4 baada ya Ewura kushusha bei ya petroli kwa Sh202.37 kwa lita ambayo ni sawa na asimilia 9.17, dizeli kwa Sh173.49 ambayo ni sawa na asilimia 8.32 na mafuta ya taa kwa 181.37, sawa na asilimia 8.70.

Hata hivyo, wakati baadhi ya makampuni yakificha bidhaa hiyo, taarifa zinasema wamekuwa wakipanga na kuzungumza kuhusu kufanya mgomo huo baridi.

Kutokana na idadi kubwa ya wafanyabiashara kusitisha kuuza mafuta, vituo vichache vilivyotii agizo la Serikali jana vilikuwa na misururu mirefu kiasi cha kuweka ‘kanuni’ za uuzaji.

Kwa mfano katika Kituo cha Big Bon, Sinza hakuna aliyeruhusiwa kununua mafuta ya Sh 10,000 ili na wengine wapate. Pia kuna kituo kingine cha mafuta cha GBP ambako kulionekana kuna misururu mirefu ya wateja.

Hali katika kituo hicho ilikuwa tete kwani foleni ilikuwa kubwa na kufanya watumiaji wengine wa njia hiyo kushindwa kupita.

Foleni kutoka katika kituo hicho kilichopo Sinza Mori ilifika mpaka Palestina hadi mchana baada ya wahudumu kusitisha uuzaji kutokana na ghasia ambazo zilisababishwa na watu waliokuwa wakilazimisha kununua mafuta kwa kutumia ‘vidumu’.
Vituo vingi katika maeneo ya Tabata vilikuwa vikiuza mafuta ya taa na dizeli tu bila ya petroli.

Tamko la Taomac

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Toamac, Salum Bisalala alikanusha kuhusu suala la wafanyabiashara kupanga bei akisisitiza vikao vya Ewura ndivyo vinavyowakutanisha katika kujadili mipango ya serikali kwenye uagizaji wa bidhaa hizo.

Bisarara alilalamika kwamba wakiuza kwa kutumia bei elekezi ziliyotolewa na Ewura, wafanyabishara wanapata hasara ya Sh150 mpaka 250 kwa kila lita ya mafuta wanayouza.

Msemaji wa umoja huo Salum Bisalala alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa, sheria inakataza wanachama wa umoja huo kukaa pamoja na kujadili masuala ya bei za mafuta na kwa hivyo isingiwezekana kwa wao kukaa kwani kitendo hicho ni kinyume na sheria.

Bisalala alisema kuwa, kufuatia utekelezaji wa bei mpya za mafuta zilizoanza kutumika mwanzoni mwa mwezi huu, makampuni yalijikuta yakiuza katika bei ya hasara jambo ambalo hata hivyo lilipokekelewa kwa mtizamo tofauti kutoka kampuni moja hadi nyingine.

“Baada ya kutangazwa kwa bei mpya kampuni zilijikuta zikipata hasara ya kati ya shilingi 150/- na 250/- kwa kila lita. Baadaye makampuni yalikuwa na mkutano kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini pamoja na EWURA kwa ajili ya kujadili suala hili. Katibu Mkuu aliyaomba yaendelee kuuza kwa bei ya hasara wakati suala hilo likitafutiwa ufumbuzi,” alieleza.

Kwa mujibu wa Bisalala wawakilishi wa makampuni walimwomba Katibu Mkuu awape muda ili waweze kuwasiliana na wakubwa zao kabla ya kutoa jibu la ndiyo au hapana kuhusiana na pendekezo hilo.

“Baada ya hapo kila mwakilishi aliwasiliana na wakuu zake. Mwakilishi wa Engen aliambiwa na wakuu wake anaweza kuuza kwa bei ya hasara kwa masaa 24. Lakini baadhi ya vyombo vya habari viliripoti vibaya kuwa aliipa serikali masaa 24 kurekebisha bei jambo ambalo siyo la kweli hata kidogo.

Baadhi ya vyombo vya habari vilikwenda mbali zaidi na kusema kuwa mwakilishi wa Engen likaidi agizo la serikali na pia aliyashawishi makampuni mengine kugoma kuuza mafuta. Hili nalo si kweli kwani sheria kama nilivyosema hapo awali hairuhusu makampuni haya kujadili suala la bei za mafuta,” alifafanua

Alifafanua kwamba, kuna tofauti kutoka kwa kampuni moja ya mafuta hadi nyingine na kuongeza kuwa yapo makubwa na madogo na hata uwezo wao pia unatofautiana na ndiyo sababu kila kampuni lilipokea suala la bei kwa mtazamo wake.

Kwa upande wake mwakilishi wa Engen Seelen Naidoo, anayetuhumiwa kuipa serikali saa 24 iwe imefidia hasara yao, alisema kuwa kilichotokea ni kuwa yeye kama msimamizi wa utendaji wa kampuni hiyo katika kazi za kila siku alipewa ruhusa ya kuuza kwa bei ya hasara kwa saa 24 tu na huo ulikuwa ni msimamo wa kampuni yake akisisitiza haukuwa na uhusiano wowote na makampuni nyingine.

“Hasara ya kati ya 150/- hadi 250/- kwa lita siyo ndogo. Wakubwa zangu walisema uwezo wetu wa kuuza kwa hasara ni saa 24 kwa sababu tungeedelea zaidi ya hapo tungeweza kupata hasara kubwa zaidi na hata kulazimika kufunga biashara maana tungekuwa tunakula mtaji,” alifafanua.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...