Wanaharakati wapenyeza ujumbe WEF





PAMOJA na kuzuiwa kuandamana kwa lengo la kufikisha ujumbe wa kuzitaka nchi tajiri kuongeza fedha hadi dola 20 milioni kwa kwa mwaka ili kusaidia waathirika wa Ukimwi, malaria na kifua kikuu, wanaharakati wa mapambano dhidi ya magonjwa hayo, jana walijipenyeza na kufikisha ujumbe wao kwa viongozi hao wa dunia.

Mbali na kuwepo kwa ulinzi mkali katika eneo unapofanyika mkutano wa uchumi duniani barani Afrika wanaharakati hao walijipenyeza kama washiriki wa mkutano huo kwa kundi dogo la watu wasiozidi 15, wakijumuia nchi zaidi ya kumi za Afrika.

Kujipenyeza kwa wanaharakati hao kulifanyika majira ya mchana ambapo pia walifanikiwa kufikisha ujumbe wao kupitia kwa balozi wa malaria, Yvonne Chakachaka pamoja na mkurugenzi wa mahusiano ya nje wa shirika la kimataifa la Global Fund, Christopher Ben.

“Ingawa tulizuiwa kuandamana, lakini tumefanikiwa kufikisha ujumbe tuliokusudia kwa viongozi wa dunia kupitia kwa balozi wa malaria na afya ya mama na mtoto, Yvonne Chakachaka na Christopher Ben mkurugenzi wa mahusiano ya nje wa Global Fund,” alisema mmoja wa wanaharakati hao Richard Shilamba mkurugenzi wa shirika lisilo la serikali la Children Education Sociaties la Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa, "tunataka nchi tajiri ziongeze fedha kwa ajili ya mapambano ya ukimwi, malaria na kifua kikuu kwa nchi za afrika kufikia dola 20milioni kila mwaka na kuacha mpango wao wa kusitisha utoaji fedha hizo.” Imeandikwa na Exuper Kachenje. SOURCE: MWANANCHI.

Comments