Wednesday, May 19, 2010

PROGRAMU YA MAFUNZO YA UONGOZI KWA JESHI LA POLISI




The IGP and the British High Commissioner, Diane Corner; Picture named (Round-table discussion) shows the British High Commissioner, Diane Corner (right) listening to the IGP and left is an official from DFID.

***************************************************************************************
Wiki hii Balozi wa Uingereza hapa nchini, Diane Corner, pamoja na Inspecta Generali wa Polisi, (IGP) Saidi Mwema wamezindua programu ya mafunzo ya uongozi kwa Jeshi la Polisi la Tanzania inayodhaminiwa na Serikali ya Uingereza. Mafunzo hayo, ambayo yataendeshwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Kuboresha Idara ya Polisi ya Uingereza (NPIA) pamoja na ile ya Hampshire kwa muda wa miezi tisa (kuanzia mwezi ujao), yatakuwa na lengo la kubadilishana uzoefu na mbinu bora - kwa kujikita zaidi katika masuala ya kiuongozi na kimenejimenti.

“Mafunzo hayo ni muhimu sana kwetu hasa kwa kipindi hiki cha maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao, lakini pia ni muhimu zaidi katika jukumu zima la kudumisha amani hapa nchini,” alishukuru IGP Saidi Mwema.

Ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mafunzo hayo, hivi karibuni Ubalozi wa Uingereza uliwapeleka kuhudhuria mafunzo huko NPIA na Hampshire nchini Uingereza IGP Saidi Mwema pamoja na maafisa wengine wa Jeshi la Polisi la Tanzania, ambao ni Kamishna wa Polisi anayeshughulikia Utawala na Rasilimali, Clodwig Mtweve, Mkuu wa Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Abdulrahman Kaniki na Kamanda wa Chuo cha Polisi Dar es Salaam, Elice Mapunda.

Ujumbe huo ulipata mafunzo huko NPIA katika masuala ya utekelezaji oparesheni za kipolisi kwa kuzingatia haki za binaadamu, utoaji huduma za kipolisi, uchunguzi, utafiti na masuala mbalimbali ya kiutawala. Pia walipata fursa ya kujiunga na jeshi la Polisi Hampshire na kufanya doria, pamoja na kujenga ujirani mwema na jamii zinazozunguka. Uzoefu huu umewezesha kujenga ushirikiano wa karibu zaidi kati ya Jeshi la Polisi la Tanzania na Hampshire, na hivyo kupanua wigo wa kujifunza kutoka pande zote mbili.

"Ninayo furaha kubwa kuzindua programu hii ya Polisi. Mafunzo haya ni mchango mkubwa katika maboresho ya sekta ya sheria, ambayo sisi pamoja na Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza (DFID) tunafadhili. Ninatumaini ya kuwa mafunzo haya yatakuza ushirikiano baina ya Jeshi la Polisi la Tanzania na lile la Uingereza ambao kila upande utakuwa na mengi ya kujifunza kutoka kwa mwenzake,” alisema Balozi Corner.
___________________________________________________________________________

No comments: