Tuesday, May 25, 2010

Tanesco yapata mkurugenzi mpya



BODI ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) imemteua Mhandisi William Mhando kuwa mkurugenzi mkuu mpya wa shirika hilo na mteule huyo ameahidi kupambana na tatizo la mikataba mibovu.
Taarifa iliyotolewa jana na Tanesco imeeleza kuwa uteuzi huo wa kuziba nafasi hiyo moto iliyoachwa wazi na Dk Idris Rashid ,unaanza rasmi Juni mosi, mwaka huu.
"Nashukuru kwa uteuzi huo, lakini najua nina challenge (changamoto) nyingi. Kuna mambo mengi ya kuwafanyia wananchi ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika," alisema Mhando alipoongea na Mwananchi jana baada ya uteuzi huo.
"Changamoto nyingine ni usambazaji wa umeme vijijini, kuboresha huduma kwa wateja na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya shirika."
Mkurugenzi huyo mpya aligeukia matatizo ya shirika hilo na kusema kuwa atahakikisha mikataba yote mibovu inapatiwa ufumbuzi na kuweka mkakati wa kudhibiti isijirudie baada ya Tanesco kukumbana na kashfa ya mkataba inayokula fedha za walipa kodi kama ya IPTL na ule uliotingisha nchi wa Richmond Development LLC.
Pia kwa sasa iko kwenye mgogoro wa mkataba wa ugavi wa nguzo za umeme na kampuni ya Sao Hill, ambayo ilikuwa ikilaumiwa kwa kushindwa kutimiza malengo ya kuzalisha nguzo zaidi ya 9,000 hadi kufikia Machi 31.
Mhando ameteuliwa kushika nafasi hiyo akitokea katika kitengo cha usambazaji umeme na masoko cha shirika hilo ambako alikuwa meneja mkuu.
Uteuzi wa Mhando unafikisha ukingoni vita kubwa iliyoripotiwa kuwepo baina ya bodi ya wakurugenzi na menejimenti ya Tanesco, ambazo zilikuwa zikidaiwa kuwa kila moja ilitaka mtu wake arithi nafasi ya Dk Idris ambaye aliachia ngazi ghafla Septemba 2009 baada ya awamu yake ya kwanza kumalizika. SOURCE:MWANANCHI

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...