Wednesday, December 30, 2009

MAKAZI YA GAVANA WA BENKI KUU TAARIFA KUHUSU UJENZI WA MAKAZI YA VIONGOZI WAKUU WA BENKI KUU YA TANZANIA


GAVANA WA Benki Kuu na manaibu wake kwa mujibu wa mikataba ya kazi zao, wanastahili kupewa nyumba ya kuishi kila mmoja. Hapo awali Gavana alikuwa anaishi Barabara ya Mahando kiwanja namba 387Masaki na Naibu Gavana Barabara ya Msese kiwanja Namba 43.

Awali Benki Kuu ilikuwa na viongozi wakuu wawili, Gavana na Naibu wake mmoja. Baada ya mabadiliko ya Sheria ya mwaka 2006, Benki Kuu ina viongozi wakuu wanne; Gavana na Manaibu wake watatu. Kila mmoja wao, kwa mikataba iliyowekwa anastahili kupata nyumba ya kuishi.

Mwaka 2006, kabla ya uteuzi wa viongozi wa sasa wa juu, Benki Kuu ilifanya uamuzi wa kujenga nyumba mbili zaidi kwa makazi ya viongozi walioongezeka. Iliamuliwa nyumba hizi zijengwe kiwanja namba 57 Barabara ya Mtwara Crescent na kiwanja namba 12 Barabara ya Tumbawe maeneo ya Oysterbay.Viwanja vyote viwili vilikuwa ni mali ya Benki Kuu vilivyokuwa na magofu yaliyopigwa marufuku kuishi wanadamu (condemned).

Timu ya wataalamu waelekezi ikiongozwa na M/S SKY Architects Consultants iliajiriwa kutengeneza michoro na ramani za nyumba hizo. Michoro miwili ilichaguliwa, moja kwa kila nyumba ili wataalamu hao watengeneze ramani kamili ya ujenzi. Nyumba zote mbili zilipangwa ziwe za ghorofa moja, vyumba vitano vya kulala, wenyeji na wageni, sebule ya wageni, sebule ya familia, mahali pa kulia na vyoo na mabafu yanayoendana na idadi ya vyumba. Majengo ya nje ni pamoja na nyumba ya kuishi watumishi, gereji ya magari, bwawa dogo la kuogelea, ukuta na vyombo vya usalama na kibanda cha walinzi.

Huduma zilizogharimiwa katika ujenzi wa nyumba hizi ni pamoja na mashine ya umeme (generator), mashine ya kupoza hewa na matenki ya kuhifadhi maji. Wakati huohuo, shughuli zingine zilizofanyika ilikuwa ni kutengeneza mahali pa kuegesha magari pamoja na bustani.

Wataalamu hawa baada ya uchoraji huu walifanya tathmini ya vifaa vinavyohitajika na maelekezo kwa wazabuni ili itumike kualika zabuni. Taratibu zote za manunuzi zilifuata sheria ya manunuzi katika kuwaalika wazabuni na kuteua wakandarasi. Kila nyumba ilikuwa ni mradi unaojitegemea na kila moja ilifanyiwa zabuni peke yake.

Izingatiwe kuwa ujenzi wa nyumba hizi ulipangwa na kuamuliwa kabla ya uteuzi wa Profesa Benno Ndulu kujiunga na Benki Kuu Septemba 2007.

Tangazo la kuwaalika wazabuni kwenye kiwanja namba 12 Barabara ya Tumbawe lilichaapishwa katika gazeti la Daily News la Februari 26,2008.Wakandarasi wote wa daraja la pili au la juu zaidi walialikwa kuwasilisha zabuni na walitakiwa kulipa ada ya shilingi 50,000. Wakandarasi 12 walituma maombi na kuchukua hati za zabuni.Lakini kati ya hao 10, waliwasilisha maombi yao kabla ya kufikia tamati ya kupokelewa maombi hayo Machi 25,2008.

Zabuni hizi zilifunguliwa na Bodi ya Zabuni ya Benki Kuu na kufanyiwa tathimini ikishirikisha mtaalamu mwelekezi wa mradi huo na Idara ya Miliki ya Benki Kuu. Mapendekezo kutoka kwa wakandarasi yalikuwa na viwango vya gharama kuanzia Shilingi 1,399,184,549.00 hadi shilingi 1,847,763,537.00 kwa kiwango cha juu. Baada ya tathmini ya zabuni hizo na kufanya masahihisho ya tarakimu zilizowasilishwa, mzabuni aliyeshinda kwa kuwa na gharama ya chini kuliko wote alikuwa ni M/S Eletrics International Co. Limited. Gharama yake baada ya masahihisho ilikuwa ni Shilingi 1,274,295,025.26.

Taarifa ya tathimini hiyo ilipitia tena kwenye Bodi ya Wazabuni na ndipo ilipofikia uamuzi wa kumteua M/S Eletrics International Co. Limited kwa bei ambayo haitabadilika (fixed price) ya Shilingi 1,274,295,025.26 ya kukamilisha ujenzi huu katika wiki 32.Mkataba wa ujenzi na mkandarasi huyo ulitiwa sahihi Juni 03,2008 na kazi ya ujenzi ikaanza mara moja. Mkandarasi huyu aliteuliwa na Bodi Zabuni (DSM) ya Benki Kuu ikaridhia kuwa M/S Remco (International) Limited ishughulikie maswala aya vipoza hewa; M/s Ginde EAP Services Ltd ishughulikie maswala ya maji safi, mabomba na maji taka na M/s Pomy Engineering Co.Ltd ishughulikie maswala ya umeme. Makampuni yote hayo yamesajiliwa Tanzania.

Wazabuni wa nyumba Namba 57 Mtwara Crescent nao pia walialikwa kwa mfumo huohuo wa ushindani wakianza na wakandarasi watano (5) ambao waliwasilisha maombi yao na kuishia na uteuzi wa M/s Holtan Builders Ltd ambayo gharama yake ya Shilingi 1,272,348,512.00 (fixed price) ilikuwa ni ya chini kuwashinda wengine na makubaliano ya kukamilisha ujenzi katika muda wa wiki 24. Mkandarasi huyo alitumia kampuni zifuatazo kwa shughuli zingine: M/s Jandu Construction & Plumbers Ltd kwa shughuli za mabomba, maji safi, na maji taka, M/s Barkley Electrical Contractors Ltd kwa maswala ya umeme na M/s Remco (International) Ltd kwa shughuli za vipoza hewa. Mkandarasi ndiye mlipaji wa gharama za shughuli hizi zote zinalipiwa kutokana na gharama ileile iliyokubalika kwa mkandarasi mkuu.

Watendaji wote wa miradi hii wanaonyeshwa kwenye mabango ambayo bado yapo kwenye viwanja hivyo. Uteuzi wa Gavana Ndulu, Manaibu Gavana, Dkt. Enos Bukuku na Bw.Lila Mkila ulifanyika wakati mipango ya awali ya kujenga nyumba hizi

ilikuwa imeshaanza. Benki Kuu ilikodisha nyumba mbili, mojakiwanja namba 480 Barabara ya Bray, Masaki na nyingine kiwanja namba 591,Msasani Peninsular kwa matumizi ya viongozi hao wawili ambao walikuwa bado wanaishi kwenye nyumba zao mbali na ofisi.

Kati ya Oktoba 2007 aliporipoti kazini kama Naibu Gavana hadi Aprili 2008, Profesa Ndulu aliishi kwenye nyumba yake iliyoko Mbezi Beach, na Naibu Gavana Mkila naye pia aliishi nyumbani kwake kabla ya kuhamia kwenye nyumba hizi zilizokodishwa.

Benki Kuu iliamua kumhamisha Naibu Gavana Juma Reli kwenda Barabara ya Mahando Masaki ili kuruhusu matengenezo ya nyumba aliyokuwa anaishi Kinondoni Barabara ya Msese. Naibu Gavana Dkt.Bukuku anaishi kwenye nyumba yake na Benki Kuu inatoa posho ya nyumba kulingana na mkataba.

Nyumba hizo mbili zilizojengwa chini ya miradi iliyotajwa, sasa hivi zimekamilika.Gavana wa Benki Kuu, Profesa Ndulu alihamia nyumba namba 12 Barabara ya Tumbawe Desemba 17,2009 na Naibu Gavana Mkila alihamia nyumba namba 57 Mtwara Crescent Desemba 4,2009

Kama ilivyo kiutaratibu, ukaguzi wa mahesabu yanayohusu miradi hiyo utafanyika kisheria. Kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006, Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) ndiye mkaguzi wa mahesabu ya Benki Kuu; ambaye ameanza kufanya kazi hii tangu mwaka 2007. Yeye ameiteua kampuni ya Ernst & Young kama wakaguzi wa kumsaidia kutekeleza jukumu hili.

IMETOLEWA NA IDARA YA UHUSIANO NA UMMA NA ITIFAKI
BENKI KUU YA TANZANIA
SEPTEMBA 30, 2009

1 comment:

obat aborsi said...

Interesting article and I Banget Fill It Love
Fraternal greetings from our.

obat aborsi

obat telat bulan

jual obat aborsi

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...