Maafa ya mafuriko





Pichani baadhi ya wakazi wilayani Kilosa mkoani Morogoro wakivuka katika eneo lililokumbwa na mafuriko yaliyoikumba wilaya hiyo kutokana na mto Mkondoa kufurika maji.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametuma salamu za pole kwa wakuu wa mikoa minne ambayo imekumbwa na maafa yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.

Aidha, Rais Kikwete amepongeza jitihada zinazofanywa na uongozi katika mikoa hiyo kukabiliana na maafa yanayosababishwa na mvua hizo.

Rais Kikwete ametuma salamu hizo za pole leo, Jumanne, Desemba 29, 2009, kwa wakuu wa Mikoa ya Dodoma, Morogoro, Ruvuma na Rukwa.

Katika mikoa hiyo, baadhi ya watu wamepoteza maisha kutokana na mafuriko, wengine wamejeruhiwa kutokana na radi, na kumekuwepo na upotevu wa mali, na mamia ya watu kukosa mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuezuliwa na upepo ulioambatana na mvua kubwa.

Katika salamu hizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhandisi Dkt. James Alex Msekela, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Luteni Kanali (mst) Issa Saleh Machibya, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mheshimiwa Christine G Ishengoma, na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mheshimiwa Daniel Ole Njoolay, Rais Kikwete amesema kuwa amesikitishwa na upotevu wa maisha, upotevu wa mali na hasara ya watu kuezuliwa nyumba zao.

“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na maafa ambayo yameambatana na mvua zinazoendelea kunyesha katika Mkoa wako. Nakupa salamu za pole wewe binafsi Mkuu wa Mkoa, na kupitia kwako, natoa mkono wa pole kwa watu wote waliopatwa na maafa kutokana na mvua hizo,” amesema Rais Kikwete katika sehemu ya salamu zake kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Kanali Machibya.


Rais ametuma salamu zenye ujumbe kama huo kwa Mhandisi Dkt. Msekela, Mheshimiwa Ishengoma na Mheshimiwa Njoolay.

Katika Wilaya ya Kongwa ya Mkoa wa Dodoma watu 220 hawana mahali pa kuishi wakati idadi ya wasiokuwa na mahali pa kuishi katika Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro imefikia 2, 152 kufuatia nyumba zao kuezuliwa ama kuharibiwa na upepo ama mafuriko. Katika wilaya hiyo hiyo ya Kilosa, nyumba 922 zimefurika maji.

Katika Mkoa wa Rukwa, watu 27 wamelazwa katika Kituo cha Afya cha Kakese baada ya kuwa wamepigwa na radi katika tukio ambako mtu mmoja amepoteza maisha.

Katika salamu zake, Rais Kikwete amewaelekeza wakuu hao wa mikoa kuendelea kuchukua hatua za dharura kukabiliana na maafa yanayotokana na mvua hizo na kuahidi kuwa Serikali yake iko pamoja na wananchi waliopatwa na maafa katika mikoa hiyo.


Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

29 Desemba, 2009

Comments