Gavana: Tumejenga nyumba mpya



Ramadhan Semtawa

GAVANA wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu amekiri benki hiyo kutumia zaidi ya Sh1 bilioni za walipa kodi kwa ajili ya kutengeneza makazi yake.

Prof Ndulu, ambaye alikuwa akitoa ufafanuzi wa habari iliyochapishwa na Mwananchi kuwa taasisi hiyo kuu ya fedha ilikarabati nyumba hiyo kwa Sh1.4 bilioni, alihusisha taarifa hizo za ubadhirifu huo wa fedha za walipa kodi na mtandao wa wafanyakazi wake ambao alisema una lengo la kumchafua.

Lakini Ndulu alisema pamoja na kutokuwepo na usahihi kwenye taarifa kwamba nyumba anayoishi ilikarabatiwa kwa kiasi hicho cha fedha, makazi anayoishi yalijengwa upya baada ya nyumba zilizokuwepo awali kubomolewa na akadokeza kuwa gharama zinaweza kuwa kubwa zaidi.

“Nyumba haijakarabatiwa, imejengwa from the ground (kutoka chini)... ni tofauti kukarabati na kujenga nyumba mpya huu ni upotoshaji wa wazi na kujaribu kuchafua mema,” alilalamika gavana huyo.

“Napenda taarifa sahihi ambazo hazipotoshi ukweli, kwa maana taarifa kama hizo zinaharibu kila kitu kizuri na kujengwa taswira mbaya kwa wananchi, kitu ambacho si sahihi.

“Pia si kweli kuhusu hizo gharama kwani hakuna tathimini kamili ambayo imekamilika hadi sasa.”

Mwananchi iliripoti kuwa nyumba anayoishi sasa gavana huyo ilikarabatiwa kwa takriban Sh1.4 bilioni na kwamba zote zilikuwa kwenye mradi wa kukarabati nyumba za vigogo wanne wa BoT; ya Ndulu na manaibu wake watatu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nyumba nyingine ni pamoja na aliyokuwa akiishi gavana wa zamani, marehemu Daudi Balali ambayo Prof Ndulu alidaiwa kuikataa kwa kuwa haina bwawa la kuogolea.

“Nashangaa kuambiwa nimekataa kuhamia kwenye nyumba; kisa haina bwawa la kuogolea, huu ni upotoshaji. Kama ni kuogelea, mimi niliogelea hadi kwenye mito, sasa sijui hili linatoka wapi,” alihoji Profesa Ndulu.

“Kwanza hiyo nyumba wanayosema ilikuwa kwa ajili ya kuishi mimi nikaikataa kwa sababu haina bwawa la kuogolea, ni uongo kwani ile alikuwa akiishi marehemu Ballali na ilikarabatiwa kwa ajili ya (Naibu Gavana Juma) Reli... sasa sijui mimi nimeingiaje,” alihoji.

Akitoa ufafanuzi wa maeneo halisi ya nyumba hizo, Profesa Ndulu alisema makazi yake hayako karibu na katibu mkuu mstaafu wa CCM na kwamba anayeishi huko ni Naibu Gavana (Taaasisi za Fedha na Mabenki) Rila Mkila.

Alisema Naibu Gavana (Uchumi), Dk Enok Bukuku hajahamia kwenye nyumba yoyote ya BoT na kwamba anaishi kwake hadi sasa.

Prof Ndulu, ambaye taasisi yake imelalamikiwa kwa kujiidhinishia mamilioni ya fedha za mikopo yenye tofauti kubwa ya viwango baina ya wafanyakazi wa chini na vigogo, alilalamika kuwa taarifa za ufujaji wa fedha katika ukarabati wa nyumba hizo zinamuweka katika kundi la mafisadi na kwamba ni mkakati wa mtandao huo alioutuhumu kuwa unaundwa na watumishi wa BoT na baadhi ya watu walio nje.

Alidai kuwa miongoni mwa watu walio nje ambao wanaeneza sifa mbaya dhidi yake ni mwanasheria maarufu ambaye anadaiwa kutangaza vita naye baada ya kuzuia mianya ya ufisadi.

Gavana Ndulu, ambaye aliteuliwa baada ya Balali kuachishwa kazi, alisema kamwe hatasita kutekeleza majukumu yake kwa ajili ya kufurahisha au kuhofu watu wenye dhamira ovu.

“Najua, kuna watu wanafikiri watanitisha au kunikatisha tamaa. Nasema nitaendelea kushikilia uzi ule ule kusimamia sheria na taratibu katika kuongoza benki na si vinginevyo,” alisema.

Alilalamika kuwa kuna watu wanataka kuzorotesha juhudi za kujengea nidhamu ndani ya taasisi hiyo na kwamba kwa dhamira zao wanaweza kukaa na kupotosha mambo kwa makusudi.
Kuhusu tuhuma nyingine kwamba, viwanja hivyo vilinunuliwa, Ndulu alisema vyote vimekuwa mali ya BoT kwa muda mrefu na hakuna hata kimoja kilichonunuliwa karibuni.

BoT imekuwa ikiangaliwa kwa karibu tangu kuibuka kwa kashfa ya wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), kashfa ambayo ilihusisha wizi wa zaidi ya Sh133 bilioni.

Taasisi hiyo pia imekumbwa na kashfa nyingine kama za bima ya maghorofa yaliyo jijini Dar es salaam na Zanzibar, kuongeza gharama katika uchapishaji wa noti na matumizi mabaya ya madaraka katika ujenzi wa maghorofa pacha.
Wafanyakazi wa benki hiyo wamejikuta kwenye kashfa za kufanikisha njama za wizi, kuajiriwa kwa kutumia vyeti vya kughushi na tuhuma za watoto wa vigogo kupewa ajira za upendeleo.

Comments