TAMKO LA BALOZI ZA KANADA, JAPAN, NORWAY NA MAREKANI KUHUSU ZOEZI LA KUANDIKISHA WAPIGA KURA ZANZIBAR
13 AGOSTI 2009
Sisi Mabalozi wa balozi zilizoorodheshwa hapo juu, tunapenda kusisitiza kuwa haki ya kupiga kura ni msingi muhimu wa demokrasia. Ni wajibu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha kuwa Watanzania wote wanapata haki hii wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Mabalozi wanasikitishwa sana na yale yanayoonekana kutia dosari na kuvuruga zoezi la uandikishaji wapiga kura huko Zanzibar. Tunasikitishwa sana, hususan, na taarifa kwamba raia wengi wa Tanzania waliopo Pemba wanakabiliwa na vikwazo katika kupata vitambulisho vya Ukaazi wa Zanzibar, ambavyo vimekuwa ni sharti muhimu la wao kuweza kuandikishwa kama wapiga kura visiwani Zanzibar, na kwamba utoaji wa vitambulisho hivyo ni zoezi lililogubikwa na hali ya upendeleo (irregular influence).
Mabalozi wanazitarajia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha kuwa hatua zote muhimu zinachukuliwa ili kurekebisha kasoro hizi zinazojitokeza hivi sasa katika zoezi la kuandikisha wapiga kura. Hatimaye mabadiliko hayo yalenge katika kuhakikisha kuwa hakuna Mtanzania yeyote, ikiwa ni pamoja na Mzanzibari, atakayenyimwa haki ya kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka 2010.
Wakati huo huo, Mabalozi, wanavihimiza vyama na vikundi vyote vya kisiasa kujizuia dhidi ya vitendo vyovyote vya utumiaji nguvu na badala yake vitumie njia za amani katika kutoa maoni na malalamiko yao.
Tamko hili limetolewa na Mabalozi wa Canada, Japan, Norway na Marekani nchini Tanzania.
Tamko hili limetayarishwa kwa pamoja na Mabalozi wa Nchi zote Wanachama wa Jumuiya ya Ulaya nchini Tanzania: Ubelgiji, Denmark,Kamisheni ya Jumuiya ya Ulaya, Finland, France, Ujerumani, Ireland, Italy, Uholanzi, Hispania, Sweden kama rais wa Jumuiya ya Ulaya na Uingereza
1 comment:
MUNGU AJAALIE WAWE NA IMANI HIYO HIYO KUZUWIYA HILA ZA WACHACHE WANAOTAKA KUHODHI MADARAKA KAMA NI WAO PEKEE WENYE HAKI KATIKA HII DUNIA.
Post a Comment