Tuesday, April 21, 2009

Bajaj sasa ruksa


Muswada uliolenga kuruhusu bajaji zitumike kama vyombo vya usafiri nchini umepitishwa rasmi kuwa sheria.

Sheria hiyo ya Leseni za Usafiri ambayo ilikuwamo katika muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2009, umesainiwa rasmi na rais kuwa sheria Nmba 3 ya mwaka 2009.

Baadhi ya miswada hiyo iliyoidhinishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa sheria kuwa ni pamoja na Sheria ya Vyama vya Siasa Namba 7 ya mwaka 2009 na Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009.

Spika wa Bunge Samuel Sitta ameliambia bunge mjini Dodoma jana kuwa miswada ambayo iliyojadiliwa na kupitishwa na bunge mwezi Februari mwaka huu sasa imetangazwa rasmi kuwa sheria.

Kupitishwa kwa sheria hizo ikiwemo inayoruhusu matumizi ya pikipiki za miguu mitatu katika usafiri wa umma kutasaidia kuondoa utata uliogubika matumizi ya usafiri huo hususan katika jiji la Dar es Salaam.

Hata hivyo matumizi hayo yatategemeana kwa kiasi kikubwa na kanuni zitakazosimamia utekelezaji wa sheria hiyo ambazo zitatungwa na wizara husika.