Na Bernard James wa Mwananchi
PADRI Sixtus Kimaro (40), aliyekuwa amefungwa jela miaka 35 mwaka 2005 baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mvulana mwenye umri wa miaka 17, ameachiwa huru jana baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali hatia zote mbili na kifungo.
Akitoa uamuzi huo jana Jaji wa Mahakama Kuu, Robert Makaramba alisema amemwachia huru Padri Kimaro kwa kuwa upande wa Mashitaka haukutoa ushahidi wa uhakika kwa mashtaka anayodaiwa kuyatenda kwa kijana aliyekamatwa akiwa naye katika eneo la Changanyikeni, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Pia Jaji Makaramba alifuta amri ya awali iliyotolewa ya Mahakama iliyomtaka Padri huyo alipe faini ya Sh milioni mbili.
Jaji Makaramba alitupilia mbali hatia aliyokutwa nayo ya ulawiti akisema hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja unaoonyesha kwamba wawili hao walikuwa wakitenda jambo lililodaiwa kutendeka.
Baada ya kutolewa uamuzi huo Padri Kimaro alinyanyua mikono yake juu na macho ikiwa ni ishara ya kumshukuru mungu kwa hatua iliyofikiwa na mahakama.
Padre Kimaro alionekana kububujikwa machozi wakati Jaji akiwa amefikia katikati kusoma hukumu hali iliyomfanya atumie kitambaa kujifuta.
Awali akiwasilisha ushahidi wa mteja wake, Wakili wa Padri Kimaro alisema upande wa mashitaka ulishindwa kuwasilisha ushahidi wa kuridhisha kumuunganisha na makosa aliyodaiwa kukutwa nayo.
Padri huyo alihukumiwa kifungo hicho katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kupatikana na hatia katika mashitaka yote matatu yaliyokuwa yakimkabili ya kulawiti, shambulio la aibu na kumdhalilisha mvulana huyo.
Alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela katika kosa la kwanza la kulawiti na miaka mitano katika kosa la pili la shambulio la aibu na kumtaka mshitakiwa huyo kumlipa Sh2 milioni mvulana aliyelawitiwa. Adhabu hizo zilikwenda sambamba.
No comments:
Post a Comment