Thursday, August 30, 2007

Uwanja wa Taifa




mechi itapigwa hapa

Sh 3,000 ya zamani, sasa ghorofani

MASHABIKI watakaotaka kuona mechi ya kirafiki baina ya Tanzania na Uganda kesho wametakiwa kuwa makini wakati wa kukata tiketi ili kujua maeneo wanayotaka kukaa na nambari za viti, huku wakikumbushwa kuwa wale waliokuwa wakilipia Sh 3,000 na kusota juani, sasa wataona mechi wakiwa juu ghorofani.
Mkurugenzi wa michezo, Henry Ramadhan aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa uwanja mpya, ambao unajulikana kwa muda kama Uwanja Mkuu wa Taifa wa Tanzania, umejengwa kwa njia ambayo itatoa nafasi kwa kila mtu kuona michezo vizuri kulingana na kiasi atakacholipia.
"Kama kule (uwanja wa zamani) mtu alikuwa anasimama wakati wote wa mchezo na kupigwa na jua, kwenye uwanja mpya atakaa ghorofani sehemu ya juu kabisa na hatadhurika na jua wala mvua," alisema mkurugenzi wa michezo, Henry Ramadhan wakati akiwaonyesha wahariri wa michezo utaratibu wa kuingia uwanjani hapo jana.
"Tena ajabu ni kwamba yule atakayelipia Sh 3,000 na kukaa juu kwenye viti vya kijani, karibu na eneo la VIP, ataona mpira vizuri kabisa sawa na yule aliyelipia Sh 30,000.
"Sasa hapa tuwape nini. Huyu wa 3,000 ni sawa kabisa na yule wa Jukwaa la Kijani la Uwanja wa Taifa. Hawa watakaolipia Sh 3,000 ni theluthi moja ya mashabiki wote watakaoingia uwanjani.
"Lakini naomba muwaambie kuwa wale wenye mshawasha wa kushangilia, basi wachague sehemu ya upinde (iliyo nyuma ya maeneo ya goli yenye viti vya rangi ya machungwa) kwa kuwa huko ndiko hasa kwa washangiliaji, hata vikundi vya ngoma vitakuwa huko."
Ramadhan aliwataka mashabiki kuwa makini kununua tiketi kulingana na sehemu wanazotaka kukaa na kuzisoma vizuri kujua milango watakayoingilia, akibainisha kuwa wale watakaoingia kupitia lango kuu ni wale tu ambao watakuwa na tiketi za VIP.
"Wale watakaokuwa hawaelewi vizuri, au wataenda sehemu ambazo si zao, watakutana na watu ambao wamepangwa kuwaelekeza," alisema. "Naomba tu wawe wastaarabu wakati watakapoelekezwa la sivyo watasaidiwa na wanausalama watakaokuwepo."

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...