Thursday, August 18, 2016

WAZIRI MKUU AWAWEKA SAWA WATUMISHI WA OFISI YAKE

*Asema safari imeiva, ataka wajipange kuhamia Dodoma



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema safari ya kuhamia Dodoma imeiva na amewataka watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wajipange kisaikolojia.



Ametoa kauli hiyo jana (Jumatano, Agosti 18, 2016) alipokutana na kuzungumza na watumishi wa ofisi yake kutoka taasisi, idara na vitengo mbalimbali waliopo Dar es Salaam.



Waziri Mkuu aliwataka watumishi hao watambue kuwa uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao chimbuko lake ni agizo lililotolewa Oktoba Mosi, 1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa chama cha TANU.



“Tangu wakati huo kumekuwa na juhudi mbalimbali zilizofanyika ili kuandaa miundombinu na hata awamu ya nne ilisimamia kwa kiwango kikubwa uwekaji wa miundombinu hiyo,” alisema.



“Pia tukumbuke kauli ya Mheshimiwa Rais aliyotoa kwenye hotuba yake ya Julai 23, 2016 alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM, na akairudia tena Julai 25, kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya Mashujaa na mimi siku hiyo hiyo nikaweka msisitizo,” alisema.



“Napenda kuwatoa hofu, mambo yanaenda vizuri ila mtambue kuwa safari imeiva sasa. Kikubwa ni kwamba tutakwenda kwa awamu kama ambavyo imepangwa,” alisema.



Aliwataka watumishi hao wazidishe mshikamano miongoni mwao huku wakitambua kuwa wana dhamana ya kuwatumikia Watanzania kwa uadilifu na uaminifu. “Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu tunapaswa tutambue dhamana tuliyonayo. Tufanye kazi kwa bidii. Tuhakikishe kila kilichopangwa kinafanyika kwa ufanisi na kinafanikiwa,” alisema.







IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

2 MTAA WA MAGOGONI,

S. L. P. 3021,

11410 DAR ES SALAAM.

ALHAMISI, AGOSTI 18, 2016.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...