Monday, August 22, 2016

Dawasco Kanda ya Tabata yaendelea kutoa Vifaa kwa ajili ya wateja wanaunganishiwa huduma za maji


Na: Frank Shija, MAELEZO. 

Huduma za uunganishaji wa mabomba ya maji kupitia program ya kuunganishwa bila ya kuwepo kwa gharama za awali kwa Wateja wa Dawasco Kanda ya Tabata waendelea kushika kasi kutokana na muitikio mkubwa wa wananchi wanaoishi maeneo hayo. 

Hayo yamesemwa na Afisa Uhusiano wa Dawasco Makao Makuu Joseph Mkonya alipokuwa akijibu malalamiko ya mmoja wa wakazi wa Mtaa wa Tabata Segerea jana Jijini Dar es Salaam. 

Mkonya alisemakuwa tangu zoezi hilo kuzinduliwa wananchi waliitikia kwa kiasi ambacho ilisababisha kujitokeza kwa changamoto ya uhaba wa vifaa kwa ajili ya shughuli hiyo na kupelekea waombaji wengi kuendelea kusubiri huduma hiyo muhimu. 

“Kutokana na huduma hiyo kuwa ya bure muitikio umekuwa mkubwa hivyo kusababisha kuwepo na changamoto ya vifaa, hata hivyo suala hilo limekwishapatiwa ufumbuzi na tayari vifaa vimenunuliwa na kuanza kugaiwa kwa wananchi waliojaza fomu za maombi ya huduma hiyo”. Alisema Mkonya. 

Kwa upande wake Meneja wa Dawasco Kanda ya Tabata Bi. Victoria Masele amesema kuwa katika kanda yake zoezi linaendelea ambapo takribani wiki moja sasa wateja wamekuwa wakipatiwa vifaa kwa ajili ya zoezi la kuunganisha mabomba ya maji katika maeneo yao. 

“Mapaka sasa wateja wa Kanda ya Tabata tumeshawapa taarifa juu ya ujio wa vifaa ili waje kuvichukua kwa ajili ya kuvifanyia kazi” Alisema Victoria. 

Aliongeza kuwa tangu zoezi hili liratibiwe jumla ya wateja 1500 wamekwishaunganishwa na huduma za maji katika maeneo mbalimbali ya Kanda ya Tabata inayojumuisha maeneo ya Mabibo hadi Vingunguti. 

Kampuni ya Dawasco ambayo ndiyo msambazaji wa huduma za maji Safi Dar es Salaam, imeanzisha program ya kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma hiyo muhimu kwa kuwawezesha kuwaunganisha na huduma hiyo bila ya gharama za awali na baadaye mteja ataanza kulipia huduma hiyo kwa malipo ya Ankara ya matumizi.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...