Wednesday, August 17, 2016

Tuzo za wasanii za EATV zazinduliwa jijini Dar leo

Mkuu wa Masoko wa EATV, Roy Mbowe (kushoto) na Afisa habari wa BASATA, Aristides Kwizela (kulia) wakimsikiliza Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Nandi Mwiyombella,alipokuwa akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusiana na udhamini wa Vodacom Tanzania katika tuzo za wasanii za EATV, Wakati wa uzinduzi wa tuzo hizo zitakazowahusisha wasanii wote wa Afrika Mashariki na kufanyika Disemba 10 2016.
Afisa habari wa BASATA, Aristides Kwizela (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari(hawapo pichani)jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa tuzo za wasanii za EATV zitakafanyika Disemba 10 2016 na kuwahusisha wasanii wote wa Afrika Mashariki,Wengine katikati Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Nandi Mwiyombella,na Mkuu wa Masoko wa EATV,Roy Mbowe.
Baadhi ya waandishi wa habari na wafanyakazi wa Vodacom Tanzania na EATV wakiwa katika uzinduzi wa tuzo za wasanii za EATV zitakafanyika Disemba 10 2016 na kuwahusisha wasanii wote wa Afrika Mashariki.
 
Katika kuleta chachu ya sanaa hapa nchini kituo cha Televisheni cha East Africa(EATV)kimeanzisha tuzo za wasanii ambazo zitafanyika katika ukumbi wa Mlimani city mwezi Desemba .

Akiongea wakati wa kutangaza uzinduzi wa tuzo hizo katika mkutano na waandishi wa habari,Mkuu wa masoko wa kituo cha televisheni cha EATV,Roy Mbowe alisema kuwa tuzo hii ni kwa ajili ya wasanii wa tasnia mbalimbali na kwa kuanzia mwaka huu itawahusu wasanii wa tasnia ya muziki na filamu katika nchi za Afrika Mashariki.

“Pengine mnaweza mkajiuliza kwanini EATV imeamua kubeba jukumu hili la utoaji tuzo za EATV. Kwa wafuatiliaji wa mambo ya kimataifa watabaini kuwa vituo mbalimbali vikubwa duniani kama kilivyo kituo cha EATV vimekuwa vikitoa tuzo na sisi tukaona kwanini tusipende kazi za wasanii wa kwetu kwa kuzizawadia tuzo na kuzikuza”.Alisema

Alisema utoaji wa tuzo hizi unaanza mwaka huu na hafla ya utoaji tuzo itafanyika Desema 10 na kituo bado kinaandaa mchakato mzima wa jinsi ya kushiriki kuwania tuzo,vipengele vitakavyoshindaniwa ambavyo alidai kuwa vitatangazwa baadaye na aliishukuru kampuni ya Vodacom kwa kutoa udhamini wa tuzo hizi zenye lengo la kutoa motisha kwa wasanii .

Mbowe aliishukuru serikali kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kutoa kibali cha kuendesha zoezi hili ambalo linalenga kukuza Sanaa na kuboresha maisha ya wasanii “Tunatoa shukrani kwa serikali ya Tanzania kutuunga mkono na tutaendelea kufanya kazi na wadau mbalimbali kuboresha tuzo hii”Alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Nandi Mwiyombella alisema Vodacom inafurahi kudhamini tukio hili muhimu lenye lengo la kuwapatia motisha wasanii wa kanda ya Afrika Mashariki.

“Moja ya dhamira ya kampuni ya Vodacom ni kuibuka na kukuza vipaji ndio maana kampuni imekuwa mstari wa mbele kudhamini michezo na Sanaa kwa kuwa inaamini kupitia sekta ya michezo watanzania wengi mbali na kupata burudani inawezesha kuongeza wigo wa ajira na kampuni itaendelea kuwezesha wasanii na wanamichezo kama ambavyo hivi sasa inavyodhamini ligi ya soka ya Vodacom Premier League na mashindano ya kucheza muziki wa dansi yanayojulikana kama Dansi 100.

Afisa Uhusiano wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA),Alistides Kwizera alipongeza kituo cha EATV kwa kuanzisha wazo lenye lengo la kukuza tasnia ya sanaa nchini na aliipongeza Vodacom kwa kudhamini tukio hili.

“Serikali kupitia BASATA iko pamoja nanyi kwa kuwa imedhamiria kuinua vipaji vya sanaa na kkuwawezesha wasanii kujiajiri hivyo tutaendelea kuwaunga mkono wakati wote na natoa wito kwa wasanii kujitokeza kuchangamkia fursa hii ambayo imejitokeza kwa ajili ya kuwatangaza na kuwawezesha kujipatia mapato kupitia kazi zao za sanaa”.Alisema.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...