Benjamin Sawe-Maelezo
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inapenda kutoa ufafanuzi juu ya habari iliyoandikwa na Gazeti la Mwanahalisi Toleo Na. 353 la Agosti 22-28, 2016 kama ifuatavyo;
Hakuna mvutano wowote ambao umetokea kati ya Mamlaka na Wamiliki wa Bandari Kavu nchini juu ya kuhifadhi mizigo inayopakuliwa bandarini. Mnamo mwaka 2008/2009 bandari ya Dar es Salaam ilikuwa inakabiliwa na shehena kubwa kuliko uwezo wake na hivyo kusababisha mlundikano wa mizigo bandarini hali ambayo ingeachwa kuendelea ingesababisha ufanisi kushuka.
Kutokana na hali hiyo wadau wa bandari walikubaliana kuanzishwa kwa bandari kavu ambazo zitafanya kazi kama ‘extension of the port’ ikiwa na maana kwamba mzigo utapelekwa katika bandari hizo na kuhudumiwa kama ambavyo ungehudumiwa ndani ya bandari.
Wadau waliingia mikataba ya jinsi ya kuhudumia shehena ya magari na makontena inayopitia bandari ya Dar es salaam.
Bandari ya Dar es Salaam ina uwezo wa kuhudumia magari 3650 ndani ya bandari kwa wakati mmoja na katika kipindi cha kuanzia Juni magari yote ambayo yalikuwa ya napelekekwa kwenye bandari kavu sasa yanahudumiwa bandarini kwa kasi na ufanisi mkubwa.
Kasi ya utoaji magari bandarini imepanda na wateja wanaridhishwa na tunawataka wateja kutoa taarifa endapo itachukua zaidi ya saa 48 kabla mteja hajatoa gari ndani ya bandari tofauti na ilivyokuwa awali ambapo mteja alikuwa analazamika kulipia gharama za storage. Ujio wa meli unaongezeka kila siku hivi sasa kuna wastani wa meli 5 kila siku zinazokuja na kutoka bandarini.
Ufanisi umepanda baada ya changamoto ambazo zilikuwepo kati ya Dec-June kufanyiwa marekebisho mbalimbali na Serikali. Mapato yameongezeka kufikia shs 662.000 bilioni 2015/2016 kiasi ambacho hakijawahi kukusanywa. Lengo tulilowekewa na Serikali ni kukusanya Trilioni moja ambalo tutalifikia.
Kushuka kwa shehena kwa kiasi kikubwa kunachangiwa na kushuka kwa kiasi cha uagizaji kutoka China ambayo inatumia sana shaba kutoka Zambia na DRC na utafiti unaonyesha kwamba siyo bandari za Tanzania tu ambazo zimeathirika bali ni bandari karibu zote Afrika Mashariki na Kusini.
Mamlaka inasisitiza ushirikiano na wadau katika kuhakikisha shehena inaongezeka na bandari inafanya kazi kwa ufanisi.
Mamlaka inaamini katika kuongeza ufanisi, kukusanya mapato na ushirikiano na wadau ili bandari ziweze kutoa mchango unaokusudiwa na Serikali katika kukuza uchumi wa Tanzania na jirani zinazotegemea bandari zetu.
No comments:
Post a Comment