Wednesday, October 21, 2009

Rais Kikwete Mitambo ya IPTL kuwashwa

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WAFANYABIASHARA na wawekezaji nchini katika kongamano la kujadili fursa za utalii nchini mjini Dar es Salaam, jana, Jumanne, Oktoba 20, 2009 walimwomba Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuingilia kati matatizo ya sasa ya mgawo wa umeme kwa kuruhusu kuwashwa kwa mitambo ya kuzalisha umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, inapenda kufafanua kuwa tayari Mhe. Rais ameingilia kati kumaliza mgawo wa sasa wa umeme nchini.

Tokea majuzi, Mhe. Rais alikwishakutoa maagizo kwa Wizara ya Nishati na Madini, pamoja na Kampuni ya TANESCO, kuchukua hatua za kuhakikisha mitambo ya kuzalisha umeme ya IPTL inawashwa, haraka iwezekanavyo, na umeme unaanza kupatikana.

Kutokana na kuharibika kwa mitambo ya kuzalisha umeme ya Songas, Ubungo, mjini Dar es Salaam, na Kihansi, Mkoani Iringa, Gridi ya Taifa ina upungufu wa megawati 80, ikiwa ni megawati 20 ambazo kwa kawaida huzalishwa na Songas, na megawati 60 ambazo huzalishwa Kihansi.

IPTL kwa sasa haizalishi umeme. Lakini ina uwezo wa kuzalisha megawati 90 hadi 100. Hizi zinatosha kuziba pengo la sasa la megawati 80 katika Gridi ya Taifa, na kumaliza mgawo wa sasa wa umeme.

Ni kweli kwamba IPTL iko kwenye mchakato wa ufilisi ambao unaendelea sasa mahakamani, lakini Mhe. Rais Kikwete ameelekeza kuwa mchakato wa ufilisi mahakamani hauzii mitambo ya kampuni hiyo kuwashwa na kuzalisha umeme wakati malumbano ya kisheria yakiendelea kortini.

Katika kuhakikisha kuwa umeme unapatikana haraka iwezekanavyo, Mhe. Rais Kikwete ametoa maagizo mbalimbali kwa Wizara za Serikali kama ifuatavyo:

(a) Wizara ya Nishati na Umeme, kwa kushirikiana na TANESCO, imeagizwa kusimamisha masuala yote ya kiufundi ikiwa ni pamoja na upatikanaji haraka wa mafuta, ili umeme huo wa IPTL uanze kuzalishwa mara moja.

(b) Wizara ya Fedha na Uchumi imeagizwa kuhakikisha kuwa inatafuta fedha za kuwezesha ununuzi wa mafuta na mahitaji mengine muhimu, ili umeme uweze kuzalishwa.

(c) Wizara ya Katiba na Sheria imeagizwa kuhakikisha kuwa inasimamia masuala yote ya kisheria yanayohusu suala hilo

Katika kutekeleza maagizo hayo ya Mhe. Rais, jana, Jumanne, Oktoba 20, 2009, Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda, tayari aliitisha kikao maalum cha Mawaziri wa Nishati na Madini, Fedha na Uchumi, Katiba na Sheria, TANESCO na vyombo vingine husika katika suala hilo kujadili jinsi ya kuhakikisha kuwa umeme wa IPTL unawashwa haraka.

Kupatikana kwa umeme wa IPTL utawawezesha mafundi ambao kwa sasa wanahangaika kutengeneza mitambo ya Songas na Kihansi kuifanya kazi hiyo kwa utulivu zaidi.

Mhe. Rais Kikwete anaelewa fika matatizo yanayowapata wananchi kwa sababu ya mgawo wa sasa wa umeme, na madhara yake kwenye uchumi wa nchi. Lakini anapenda kuwahakikishia wananchi wote kuwa mgawo wa sasa wa umeme utakwisha katika siku chache zijazo.


Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

21 Oktoba, 2009

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...