Wednesday, October 21, 2009

Balozi Dk.Augustine Mahiga Kupewa TUZO



Balozi Dk. Augustine Mahiga

Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Dkt. Augustine Mahiga atatunukiwa Tuzo ijulikanayo kama ‘ “The Spirit of the United Nations” kwa mwaka wa 2009.
Balozi Mahiga anakuwa mwana-diplomasia wa tatu kutunukiwa tuzo hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007.


Waandaji na watoaji wa tuzo hiyo ni Kamati ya Taasisi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na masuala ya kiroho, maadili na mambo yanayo hususu ulimwengu katika ujumla wake (CSVGC-NY), ikishirikiana na taasisi nyingine isiyo ya kiserikali ya Umoja wa Mataifa inayo husika na masula ya mikutano na uhusiano.( CONGO)


Aidha kuanzia mwaka huu wa 2009 waandaji wa Tuzo hiyo ya “The spirit of the United nations”, wameamua iwe inatolewa kwa makundi matatu ambayo ni wana-diplomasia,wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, na wawakilishi wa taasisi zisizo za kiserikali ambazo zinauhusiano na Umoja wa Mataifa kupitia Kamati ya inayohusika na masuala ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii (ECOSOC) au Idara ya Mawasiliano ya Umma (DPI)ya Umoja wa Mataifa.


Balozi Mahiga atatunukiwa tuzo hiyo Oktoba 26 katika wiki ambayo taasisi hiyo huadhimisha wiki ya kiroho, maadili na masuala yahusuyo ulimwengu. Maadhisho ya wiki hiyo yalizunduliwa rasmi mwezi Octoba mwaka 2007 kama sehemu ya kuendeleza utamaduni wa amani kama inavyotambuliwa ndani ya katiba ya Umoja wa Mataifa.


Kwa mara ya kwanza Taasisi hiyo ilimtunuku Tuzo hiyo mwaka 2007, Balozi Anwarul K. Chowdhury, (2007) aliyekuwa kwa wakati huo Katibu Mkuu Msaidizi wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya nchi maskini na zinazoendelea, nchi zisizokuwa na bahari, na nchi zinazoendelea za visiwa vidogo.


Balozi wa Pili alikuwa ni Balozi wa Kudumu wa Ufilipino katika Umoja wa Mataifa, Hilario G. Dvide, Jr. aliyetunukiwa tuzo hiyo mwaka 2008.Watunukiwa wote hao waliteuliwa kupokea tuzo hiyo kutokana na juhudi zao za kutangaza na kuendeleza masuala kiroho na maadili katika Umoja wa Mataifa.


Wanaopatiwa tuzo hiyo ni watu ambao pamoja na sifa nyingine wanatakiwa wawe wameonyesha kwa vitendo dira na maadili ya kiroho ya Umoja wa Mataifa kama ilivyoainishwa katika katiba ya Umoja wa Mataifa na Tamko la haki za Binadamu kama msingi mkuu wa kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa.


Aidha anatakiwa awe ni mtu ambaye amefanya kazi katika Jumuia ya Umoja wa Mataifa kwa takribani miaka mitano mfululizo.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...