Tuesday, October 20, 2009

MCT yazindua jopo la wajuzi


Dk Peter Mwesige (Uganda)

Wangethi Mwangi (Kenya)

Profesa Palamagamba Kabudi


BARAZA la Habari Tanzania (MCT), jana lilizindua jopo la wajuzi la kwanza (Think Tank) lenye wajumbe sita ambao watahusika na uhuru wa kujieleza na masuala ya vyombo vya habari.

Mwenyekiti wa jopo hilo kwa miaka minne ijayo ambalo lilitambulishwa jana mbele ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini ni Profesa Issa Shivji.

Wajumbe ni Jenerali Ulimwengu, Profesa Robert White(Marekani), Profesa Palamagamba Kabudi, Dk Peter Mwesige (Uganda) na Wangethi Mwangi (Kenya).

Akizungumza wakati wa utambulisho wa jopo hilo jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa (MCT), Kajubi Mukajanga alisema kwa muda mrefu baraza hilo lilikuwa likifikiria jinsi ya kuboresha muelekeo wa vyombo vya habari hali iliyowalazimu kuunda jopo hilo chini wa wajuzi wa fani mbalimbali ili kuboresha taaluma ya habari.

“Kazi ya jopo hili ni kutafakari na kuandika machapisho, kukutana na watunga sera, kutembelea shule mbalimbali za uandishi wa habari pamoja na kuandika makala, ni wazi kuwa jopo hili litachangia fani hii kuingia katika kipindi kipya cha weredi wa tafakari mpya,” alisema Mukajanga na kuongeza;

“Kwa miezi 12 ya kwanza jopo hili litashughulikia na uhuru wa wahariri wa vyombo vya habari kwa sababu mwishi wa siku malengo ya vyombo vya habari ni kutoa habari kwa maslahi ya umma na sio kuandika habari kutokana na shinikizo la mmiliki au wanasiasa.”

Akizungumza mara baada ya kutangazwa kwa jopo hilo Profesa Palamagamba Kabudi alisema wamiliki wa vyombo vya habari hawatakiwi kuingilia utendaji wa kazi wa wahariri wao na kusisitiza kuwa wahariri wanatakiwa kupewa uhuru ili mradi hawakiuki maadili ya taaluma ya habari.

Akikinukuu kitabu kilichoandikwa na marehemu Mwalimu Julius Nyerere kinachoitwa ‘Uhuru na Umoja’, Profesa Kabudi alisema; “ Katikia kitabu hiki mwalimu alijaribu kuelezea umuhimu wa uhuru katika ngazi zote, hivyo hata mimi nasisitiza kuwa wahariri wana haki zote katika maamuzi ikiwa ni pamoja na habari gani itoke ipi isitoke.”

“Lakini uhuru huu lazima uzingatie haki za kimsingi za binadamu na kutokubali kuingiliwa katika utendaji wa kazi na mmiliki au mtu yeyote kutoka nje, lakini sio wamiliki tu wahariri pia hujikuta wanakosa uhuru kwa sababu ya wanasiasa, kutojiamini ambako huchangiwa na ukosefu wa elimu, watangazaji, kuogopa kufukuzwa kazi, wafanyabiashara pamoja na imani za kidini”

Alisema kuwa vyombo vingi vya habari kukosa sera ya kudumu, wamiliki wa vyombo vya habari kujali fedha kuliko kuelimisha umma, kuandika habari za kuwafurahisha wanasiasa ni moja ya sababu za kutoweka kwa uhuru wa wahariri.

“Kinachotakiwa hapa ni kuhakikisha wahariri na waandishi wanapata mafunzo ya mara kwa mara, kujali sera, wahariri kuwa huru katika ufanyaji wao wa kazi kutasaidia sana kuboresha taaluma hii” alisema Kabudi


Naye Mwenyekiti wa jopo hilo, Profesa Issa Shivji alisema uhuru wa mhariri wa chombo chochote cha habari ni kitu muhimu sana na kusisitiza kuwa uhuru wa vyombo vya habari hauwezi kuzungumziwa kama wahariri hawatakuwa na uhuru.

“Tatizo kubwa lipo kwa wamiliki kwani baadhi yao wamekuwa wakiingilia kazi za wahariri wao na kutokana na kuwa wahariri hawa pengine nao wanaogopa kufutwa kazi hujikuta wakifanya kazi bila uhuru kitu ambacho kinakuwa hakina maana halisi ya taaluma hii ya habari kwani lengo lake ni kuelimisha umma” alisema Shivji na kuongeza Imeandikwa na Fidelis Butahe, Picha za Mwananchi Communications.

No comments: