Thursday, October 29, 2009
Balozi Mahiga apokea TUZO
Balozi wa Tanzania Katika Umoja wa Mataifa, Dkt Augustine Mahiga akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Kamati ya Maadili na Masuala ya Kimataifa, na familia yake mara baada ya kutunukiwa Tuzo ya the Spirit of the United Nations" 2009" kulia kwa Balozi aliyeshika Tuzo ni Mke wake, Bibi Elizabeth Mahiga
Na Mwandishi Maalum
New York
Dkt Augustine Mahiga Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, amesema Tuzo aliyopewa imemwongezea ari na nguvu ya kujituma zaidi katika kutafuta amani, kutetea utu wa mwanadamu na haki za jamii na katika maeneo ambayo bado mambo hayo yanahitajika.
Ameyasema hayo wakati alipokuwa akitoa shukrani zake mara baada ya kutunukiwa tuzo ijulikanayo kama “The Spirit of the United Nations 2009” aliyotunukiwa mapema wiki hii jijini New York .
Kuhusu Tuzo hiyo aliyopewa, Balozi Augustine Mahiga mwanadiplomasia mzoefu katika Umoja wa Mataifa, anaielezea kuwa Tuzo hiyo kwamba, ni Tuzo ya Watanzania, Waafrika na wale wote wenye kuitakia dunia mema na kwamba yeye ni mpokeaji tu na mshikiliaji wa tuzo hiyo kwa niaba yao.
Akasema ataendelea kuzitafuta haki hizo za wanyonge kupitia Umoja wa Mataifa ambako anaamini kuwa mahali stahili kwa kuwa ndipo panapowakusanya kwa pamoja watu wenye fikra sawa na nia ya kuyafikia malengo mbalimbali yaliyowekwa na umoja huo.
“Umoja wa Mataifa ni chombo cha kilimwengu na cha kipekee ambapo nchi kubwa na ndogo zinakutana na kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano kama mataifa yaliyo sawa. Umoja wa Mataifa ni daraja linalounganisha tamaduni mbalimbali, rangi na imani katika kujenga utengamano , ushirikiano na maelewano ”
Tuzo hiyo ambayo hutolewa kila mwaka na Kamati ya Shirika la Maadili na Masuala ya Kimataifa , hutolewa kwa watu ambao msimamo na utendaji kazi wao katika Umoja wa Mataifa umekuwa ni kielelezo cha misingi na mwelekeo wa Umoja wa Mataifa.
Kamati ya Uteuzi ilieleza kuwa Balozi Mahiga amedhihirisha na kujitokeza kama mfano wa mtu anayeamini na kutekeleza misingi hiyo.
Tangu kuanza kutolewa kwa tuzo hiyo mwaka 2007, tayari imesha tolewa kwa mabalozi wawili wote wa Umoja wa Mataifa , wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na Taasisi zisizo za Kiserikali. Balozi Mahiga anakuwa Balozi wa kwanza kutoka Afrika kupata Tuzo hiyo.
Katika shukrani zake hizo, Balozi Mahiga akasisitiza kwamba Katiba ya Umoja wa Mataifa na Tamko la Haki za Binadamu, ni mihimili mikuu katika kukidhi nia ya mwanadamu katika kutafuta amani, maendeleo, haki, usawa na utu wa mwanadamu.
“ Hata wanao mkana Mungu hawawezi kuyapinga maadili haya ya msingi ambayo ni amani, haki za jamii, maendeleo ya mwanadamu na utu wa mtu, misingi ambayo Umoja wa Mataifa ndipo inaposimamia” akabainisha Balozi Mahiga.
Akawaeleza wageni waliohudhuria hafla hiyo kwamba katika miaka hiyo 17 akiwa mawana diplomasia ameshuhudia mambo mengi na ya kutisha yaliyomkumba mwanadamu.
Anayataja mambo hayo kuwa ni umaskini, vita na machafuko, watoto kulazimishwa kubeba silaha na kupigana , wanawake kudhalilishwa na mauaji ya halaiki na ya kimbari ya Rwanda.
“ Matukio haya ya kutisha niliyoyashuhudia katika utendaji wangu wa kazi, kwa njia moja yameniimarisha na kunifanya nielekeze nguvu zangu katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayomkabili mwanadamu kwa njia ya amani na kwa kutumia nguvu za pamoja za Kikanda, Umoja wa mataifa na watu wenye mapenzi mema.
Awali akitoa wasifu wa Balozi Augustine Mahiga , Mwenyekiti wa Taasisi iliyotoa Tuzo hiyo Bi Audrey Kitagawa, alimwelezea Balozi Mahiga kama mwanadiplomasia ambaye katika kipindi chake cha miaka 17 si tu amekuwa mstari wa mbele katika kutetea na kupigania haki za makundi mbalimbali ya jamii wakiwamo wakimbizi , wanawake na watoto lakini pia ameandika machapisho mbalimbali na kutoa mihadhara yenye mwongozo, ushauri na mapendekezo ya kukabiliana na madhira mbalimbali yanayomkabilia mwanadamu na dunia.
Miongoni mwa machapisho hayo ni Ushirikiano wa Kikanda na Utatuzi wa Migogoro ya Kivita, Upokonyaji wa Silaha na Maendeleo katika Afrika, Utatuzi wa migogoro na Usalama katika Afrika, Masuala ya wakimbizi , Haki za wanawake na watoto na ulinzi wa wananchi katika maeneo yenye vita na machafuko.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA
Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...
-
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu na timu ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa akiwa katika ...
-
NATIONAL EXAMINATIONS COUNCIL OF TANZANIA PSLE-2014 EXAMINATION RESULTS ARUSHA DAR ES SALAAM DODOMA IRINGA KAGERA KIGOMA ...
-
Adam Malima James Wanyancha Hamis Kagasheki RAIS Jakaya Kikwete ameteua Baraza la Mawaziri, huku likiwa na sura na damu mchanganyiko. Bar...
No comments:
Post a Comment