Monday, April 28, 2025

WAZIRI WA ARDHI AZINDUA MKUTANO WA WADAU KWA AJILI YA MAREJEO YA MPANGO WA UENDELEZAJI UPYA WA OYSTERBAY NA MASAKI JIJINI DAR ES SALAAM

 







Dar es Salaam, 28 Aprili 2025
Leo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi, amezindua rasmi mkutano wa kwanza wa wadau kwa ajili ya marejeo ya mpango wa uendelezaji upya wa eneo la Oysterbay na Masaki jijini Dar es Salaam. Mkutano huu ni sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa mpango kabambe wa kuboresha maeneo ya fukwe na mandhari ya asili ya maeneo hayo, na pia kuweka mazingira bora kwa maendeleo ya jiji la Dar es Salaam.

Katika uzinduzi wa mkutano huo, Mhe. Ndejembi alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wadau wote wanahusishwa kikamilifu katika kutoa maoni yao kwa uwazi na uhuru. Alisema kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, inapaswa kuhakikisha kuwa kila mdau anapata fursa ya kutoa maoni kuhusu utekelezaji wa mpango huo, huku akizingatia maslahi mapana ya jamii, hasa kwa kutambua mabadiliko ya kijamii na kiuchumi yanayotokana na kuhamia kwa makao makuu ya nchi Dodoma.

Nisisitize pia kuhakikisha uendelezaji wa fukwe na mandhari ya asili ya eneo la mpango uzingatie kanuni za uendelevu, uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisisitiza Mhe. Ndejembi.

Aidha, Mhe. Ndejembi alifafanua kuwa mpango mpya unapaswa kufungamanishwa na mpango kabambe wa maendeleo ya miji uliopo na kuzingatia miongozo ya maendeleo ya miji. Alisema kuwa sekta binafsi inapaswa kupata nafasi stahiki katika utekelezaji wa mpango huu, lakini kwa kufuata miongozo inayohusiana na kulinda haiba ya maeneo haya ya hadhi ya juu.

Waziri Ndejembi alieleza kuwa mpango huu shirikishi umetayarishwa kwa kushirikiana na Halmashauri zote na umejengwa katika Dira ya kuwa na Jiji endelevu lenye ushindani kiuchumi linalotumia rasilimali zake kiufanisi na kuhifadhi mazingira. Aliongeza kuwa mpango huo ni muhimu katika kuboresha miundombinu ya jiji na kukuza ustawi wa wananchi, huku kuhifadhi vyanzo vya maji na mazingira ya maeneo hayo.


UMUHIMU WA MPANGO HUU:

Mpango wa uendelezaji wa Oysterbay na Masaki ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Tanzania kuhakikisha kuwa maeneo ya miji yanaboreshwa kwa kufuata miongozo ya kimataifa ya maendeleo endelevu. Eneo la Oysterbay na Masaki ni miongoni mwa maeneo yenye hadhi ya juu jijini Dar es Salaam, na kuboresha miundombinu yake kutaleta manufaa makubwa kwa wakazi na taifa kwa ujumla.

Kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi na uhifadhi wa mazingira, mpango huu utajikita katika kuendeleza maeneo haya kwa njia inayozingatia maendeleo endelevu, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma bora za jamii, uboreshaji wa usafiri, na maendeleo ya kiuchumi.

No comments:

RAIS SAMIA AWASILI MSUMBIJI KWA SHEREHE ZA MIAKA 50 YA UHURU

MAPUTO – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewasili jijini Maputo, Msumbiji leo tarehe 24 Juni 2025, ...