Unguja – Zanzibar
Aprili 24, 2025
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amesema Serikali zote mbili za Muungano chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi zimejipanga kwa dhati kufanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Michezo kwa kuimarisha miundombinu ya kisasa ya michezo na kuwajengea uwezo wataalamu wa michezo ili kukuza vipaji na kuongeza ushindani wa michezo katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
Mhe. Mpango ameyasema hayo leo Aprili 24, 2025 wakati wa Hafla ya Uwekaji Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Viwanja vya Michezo vya Priz katika eneo la Kilimani, Unguja – Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
"Ujenzi wa viwanja hivi vya michezo ni mwendelezo wa juhudi za Serikali katika kuwekeza kwenye sekta ya michezo ambayo ni sekta ya kimkakati inayokua kwa kasi, na yenye uwezo wa kutoa ajira, kujenga afya ya jamii, na kutoa hamasa kwa mashindano ya kimataifa," alisema Makamu wa Rais.
Aidha, Mhe. Dkt. Mpango alibainisha kuwa Serikali kupitia Wizara husika itaendelea kuhamasisha ushiriki wa jamii katika michezo mbalimbali ikiwemo michezo ya mpira wa miguu, mpira wa pete, riadha, bao, drafti, karata, mieleka, mbio za baskeli, pamoja na michezo ya jadi kama mbio za ngalawa na mchezo wa ng'ombe.
"Serikali inalenga kutoa fursa kwa watoto, vijana, wanafunzi, wanawake na watu wenye ulemavu kushiriki kwenye michezo katika mazingira salama, rafiki na jumuishi," alisisitiza Mhe. Mpango.
Makamu wa Rais pia alieleza kuwa ujenzi wa viwanja hivyo umezingatia mahitaji ya makundi maalum, ikiwa ni pamoja na kupunguza changamoto za udhalilishaji, miundombinu isiyofikika kwa wachezaji wenye mahitaji maalum, na umbali wa kufuata huduma za michezo.
Katika kuadhimisha miaka 61 ya Muungano, Mhe. Mpango alihimiza shughuli za kuhifadhi mazingira kama vile upandaji miti kwenye maeneo ya viwanja vya michezo na matumizi ya nishati safi ya kupikia, sambamba na usafi wa mazingira.
Pia, ametoa wito kwa sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kukuza sekta ya michezo kupitia uanzishaji wa "Green Parks", timu na klabu za michezo, shule maalum za michezo, na programu za ushirikishwaji wa watu wenye mahitaji maalum.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Mhe. Tabia Maulid Mwita amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imevuka malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 kwa kuwekeza kikamilifu katika miundombinu ya michezo katika visiwa vya Unguja na Pemba. Amesema viwanja hivyo ni fursa muhimu kwa vijana kujenga maisha bora na kuepuka tabia hatarishi kama matumizi ya dawa za kulevya.
No comments:
Post a Comment