Boston, Marekani – 28 Aprili 2025
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, yuko mjini Boston, Marekani, ambako anashiriki katika kutoa mafunzo kwa Mawaziri wa Fedha na Mawaziri wa Mipango kutoka nchi mbalimbali zinazoendelea.
Mafunzo hayo yanafanyika chini ya mpango maalum wa Chuo Kikuu cha Harvard ujulikanao kama Harvard Ministerial Leadership Program, mpango unaolenga kuwawezesha viongozi waandamizi wa serikali kutoka nchi zinazoendelea kuimarisha uongozi, upangaji wa sera, na utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika nchi zao.
Katika programu hiyo, Mheshimiwa Dkt. Kikwete amealikwa kama mmoja wa Viongozi Wakuu wa Kitaifa Wastaafu kushiriki kama mkufunzi na mshauri, akitumia tajiriba yake pana katika uongozi wa taifa na ushiriki wa kimataifa kuhamasisha na kuwajengea uwezo viongozi wa kizazi kipya.
Mafunzo haya yanahusisha Mawaziri kutoka sekta muhimu za serikali wakiwemo Mawaziri wa Fedha, Uchumi na Mipango kutoka mataifa ya Afrika, Asia, na Amerika Kusini. Washiriki wanapewa mbinu bora za uongozi, usimamizi wa rasilimali, uboreshaji wa sera, pamoja na kushirikiana kwa karibu na wataalamu wa kimataifa wa uchumi, maendeleo na utawala bora.
Mbali na Rais Mstaafu Dkt. Kikwete, mpango huu pia unashirikisha:
-
Wakuu wa Taasisi za Kimataifa za maendeleo,
-
Wawakilishi wa sekta binafsi,
-
Mabingwa wa masuala ya sera za uchumi na maendeleo kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Kupitia ushiriki wake, Mheshimiwa Dkt. Kikwete anaendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuchangia maendeleo ya uongozi bora duniani, kwa kuhamasisha maadili ya utumishi wa umma, uwajibikaji na uwazi miongoni mwa viongozi wa nchi zinazoendelea.
Programu ya Harvard Ministerial Leadership imekuwa ikihusisha viongozi wa ngazi ya juu kutoka serikalini, ikiwa na lengo la kujenga msingi thabiti wa mageuzi katika sekta za afya, elimu, fedha na uchumi, kwa kutumia uzoefu halisi wa viongozi waliowahi kuongoza mataifa yao kwa mafanikio
No comments:
Post a Comment