Mjumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amehitimisha rasmi ziara yake nchini Burkina Faso kwa kukutana na Rais wa nchi hiyo, Mhe. Captain Ibrahim Traoré.
Mkutano huo ulifanyika leo, Aprili 17, 2025, katika mji mkuu wa Ouagadougou, na ulihudhuriwa na maafisa waandamizi kutoka Serikali za Tanzania na Burkina Faso.
Katika mazungumzo yao, Dkt. Kikwete alielezea furaha yake kwa kupata fursa ya kukutana na Rais Traoré na kumkabidhi ujumbe maalum kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Rais wangu amenituma nije kuwasilisha Ujumbe Maalum kwako na nimefurahi umenipa fursa hiyo na leo umeupokea rasmi," alisema Dkt. Kikwete wakati wa mkutano huo.
Mbali na kuwasilisha ujumbe, Dkt. Kikwete alitumia fursa hiyo kuwasilisha pia salamu za mshikamano na urafiki kutoka kwa Rais Samia kwa Serikali na wananchi wa Burkina Faso.
Dkt. Kikwete alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika, akisema kuwa bara hilo lina nafasi kubwa ya kujiletea maendeleo kwa kutumia ipasavyo rasilimali zake. Alisisitiza kuwa kubadilishana uzoefu kati ya mataifa ya Afrika ni jambo muhimu ili Afrika iweze kuimarisha uchumi wake kwa manufaa ya watu wake.
Kwa upande wake, Rais Captain Ibrahim Traoré alielezea shukrani zake kwa ujio wa Dkt. Kikwete na kuahidi kuendeleza mahusiano mema kati ya Burkina Faso na Tanzania. Alieleza kuwa ujumbe huo wa Rais Samia ni ishara ya udugu wa kweli wa Afrika na aliahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.
Mkutano huo umetajwa kuwa ni sehemu ya juhudi za kidiplomasia za kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya nchi za Afrika, huku Tanzania ikiendelea kushirikiana na mataifa mengine katika kukuza amani, maendeleo na ustawi wa bara la Afrika.
No comments:
Post a Comment