Na: Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Tarehe: Aprili 22, 2025
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, leo Aprili 22, 2025, amewasili mkoani Arusha kwa ajili ya kuanza ziara rasmi ya kikazi ya siku tano. Ziara hiyo inalenga kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kujadiliana na wananchi kupitia mikutano ya hadhara katika wilaya mbalimbali za mkoa huo.
Katika ziara hiyo, Dkt. Biteko anatarajiwa kutembelea na kufanya ukaguzi wa miradi muhimu inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi katika sekta za Maji, Elimu, na Afya. Aidha, atafanya mikutano ya hadhara katika wilaya za Arusha Jiji, Arumeru, Longido, na Monduli, ambapo atapata fursa ya kusikiliza changamoto, kupokea maoni ya wananchi, pamoja na kutoa mrejesho wa serikali juu ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Ratiba ya Ziara (Aprili 23–26, 2025):
-
Aprili 23: Kukagua miradi ya maji na elimu katika Wilaya ya Arusha Jiji
-
Aprili 24: Kutembelea vituo vya afya na kufanya mkutano wa hadhara katika Wilaya ya Arumeru
-
Aprili 25: Kukagua miradi ya maendeleo ya jamii katika Wilaya ya Longido
-
Aprili 26: Ziara katika Wilaya ya Monduli na kufanya mkutano mkubwa wa hadhara na wananchi
Ziara hii pia ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambapo viongozi wa kitaifa wamekuwa wakifanya ziara na mikutano kwa lengo la kufikisha ujumbe wa mshikamano, maendeleo na mustakabali wa taifa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Akizungumza mara baada ya kuwasili, Dkt. Biteko alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa miradi ya kimkakati nchini, huku kipaumbele kikiwa ni kuboresha huduma za kijamii na kuinua maisha ya wananchi hasa wa maeneo ya pembezoni.
“Tutahakikisha kwamba kila mradi unaotekelezwa unaleta matokeo chanya kwa wananchi. Hii ni dhamira ya dhati ya Serikali ya kuhakikisha rasilimali za taifa zinaleta tija kwa maendeleo ya watu wetu,” alisema Dkt. Biteko.
Ziara hii inatarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wananchi, sambamba na kutoa msukumo mpya katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea katika mkoa wa Arusha na maeneo jirani.
No comments:
Post a Comment