Luanda, Angola – 08 Aprili 2025
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameshuhudia utiaji saini wa mikataba muhimu ya ushirikiano kati ya Tanzania na Angola, ikijumuisha masuala ya ulinzi na usalama pamoja na Hati ya Makubaliano kuhusu kukuza uwekezaji. Hafla hiyo imefanyika katika Ikulu ya Luanda, mbele ya mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Angola, Mhe. João Manuel Gonçalves Lourenço.
Mikataba hii inalenga kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia, kukuza biashara na uwekezaji baina ya nchi hizi mbili, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na kiulinzi katika kuhakikisha amani na usalama wa kikanda.
Kupitia Hati ya Makubaliano kuhusu Uwekezaji, Tanzania na Angola zimeahidi kushirikiana katika maeneo ya nishati, kilimo, miundombinu, na uchumi wa viwanda, kwa kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji na kubadilishana uzoefu katika sekta hizo.
Kwa upande wa usalama, mkataba wa ushirikiano wa kijeshi utawezesha mafunzo ya pamoja, kubadilishana taarifa, pamoja na kushirikiana katika mapambano dhidi ya uhalifu wa mipakani na ugaidi.
Katika hotuba yake, Rais Samia amesisitiza kuwa ushirikiano huu wa kihistoria unatoa fursa ya kipekee kwa mataifa haya mawili kuimarisha mshikamano wa Kiafrika, kukuza uchumi, na kuhakikisha usalama wa raia wao. Viongozi wote wawili wameonesha dhamira ya dhati ya kuendelea kuimarisha uhusiano huu wa kirafiki na kimaendeleo.
Tukio hili ni sehemu ya ziara rasmi ya kitaifa ya Rais Samia nchini Angola, yenye lengo la kuimarisha diplomasia ya uchumi na kuendeleza ajenda ya Tanzania ya kukuza mahusiano ya kimataifa kwa manufaa ya wananchi.
No comments:
Post a Comment