Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, leo Aprili 29, 2025, ni mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari, yanayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Gran Melia, jijini Arusha.
Maadhimisho haya yamewaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya habari kwa lengo la kubadilishana mawazo na kufanya majadiliano ya kina kuhusu fursa na changamoto zinazoikabili sekta ya habari nchini.
Aidha, maadhimisho haya yanatoa fursa ya kuangazia nafasi ya vyombo vya habari katika kuimarisha demokrasia, uwazi, uwajibikaji na haki ya kupata taarifa, sambamba na kuhimiza matumizi ya maadili, weledi na teknolojia ya kisasa katika uandishi wa habari.
Waziri Mkuu anatarajiwa kutoa hotuba muhimu itakayogusa masuala ya sera, mazingira ya kazi kwa wanahabari, usalama wao, na hatua za serikali katika kuhakikisha uhuru na ustawi wa sekta ya habari unalindwa na kuendelezwa.
Serikali inatoa wito kwa wadau wote wa habari na wananchi kwa ujumla kuitumia siku hii kutafakari na kuunga mkono juhudi za kujenga tasnia ya habari iliyo huru, makini na yenye kuzingatia maadili ya taaluma.
No comments:
Post a Comment