Friday, September 13, 2024

WAZIRI KIJAJI AKUTANA NA KAMISHENI YA TABIANCHI YA BONDE LA CONGO

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza na Waziri wa Utalii na Mazingira wa Jamhuri ya Congo ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Kamisheni hiyo Mhe. Arlette Soudan – Nonault (kushto jijini Dar es Salaam. Wengine ni Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Bi. Christina Mndeme na Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ambaye pia ni Mwakilishi wa nchi katika Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo Prof. Dos Santos Silayo.
Waziri wa Utalii na Mazingira wa Jamhuri ya Congo ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Kamisheni hiyo Mhe. Arlette Soudan – Nonault akizungumza kwenye kikao na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji wakati wa kikao cha Ujumbe wake kutoka Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Congo na Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo jijini Dar es Salaam


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Utalii na Mazingira wa Jamhuri ya Congo ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Kamisheni hiyo Mhe. Arlette Soudan – Nonault (kulia) na Ujumbe wa Kamisheni hiyo jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, ametoa wito kwa Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Congo (CBCC) kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. 

Akizungumza wakati wa kikao na ujumbe kutoka CBCC na Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo, kilichoongozwa na Waziri wa Utalii na Mazingira wa nchi hiyo, Mhe. Arlette Soudan – Nonault, jijini Dar es Salaam, Dkt. Kijaji alisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za haraka ili kulinda dunia kutokana na changamoto hizi za mazingira.

Dkt. Kijaji alibainisha kuwa, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Tanzania imeanzisha biashara ya kaboni inayohusisha upandaji wa miti kwa wingi, hatua inayosaidia kupunguza viwango vya hewa ya ukaa. 

“Sisi kama taifa tumeanza kuchukua hatua kwenye biashara ya kaboni na tunatamani tuungane, tushirikiane na tunufaike kwa pamoja kubadilisha ujuzi ili tufikie malengo. Tunahitaji maendelezo ambayo wenzetu wamepiga hatua huku wakiharibu mazingira, na waathiriki wakubwa ni sisi nchi zinazoendelea,” alisisitiza Dkt. Kijaji.

Pia, Dkt. Kijaji aliipongeza CBCC kwa kusaidia nchi wanachama kupata fedha kutoka katika Mfuko wa Bluu na benki mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza shughuli za utalii na mazingira. Alisisitiza umuhimu wa mawaziri wanaoshughulikia mazingira kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia badala ya kuni au mkaa, ili kupunguza ukataji wa miti holela.

Katika juhudi za kuimarisha nishati safi, Tanzania tayari imeandaa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia, ambapo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amepewa ukinara wa kuhakikisha kuwa lengo la kufikia asilimia 80 ya kaya kutumia nishati safi ifikapo mwaka 2034 linatimizwa. 

Dkt. Kijaji aliwashukuru wakuu wa nchi kwa kuanzisha Kamisheni ya CBCC kwenye Mkutano wa COP22, akitambua mchango wake katika kuangalia mabadiliko ya tabianchi na mazingira kwenye Bonde la Congo.


 

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...