MKURUGENZI MKUU Aanza Ziara Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini

 

Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Hamad Abdallah akikagua maduka ya biashara eneo la Mlandege Manispaa ya Iringa na ameupongeza Mkoa wa Shirika Iringa kwa ubunifu walioufanya wa kujenga maduka hayo ya kisasa kwa muda mfupi ambayo sasa yaliingizia shirika mapato zaidi. Maduka hayo tisa kwa sasa yaliingizia Shirika mapato na kuwapa wananchi fursa za kufanya biashara.
Eneo la maduka ya biashara na nyumba za makazi lililopo Gangilonga katika Manispaa ya Iringa limetemebelewa na Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Hamad Abdallah ambaye yupo katika ziara ya kutembelea Mikoa ya Shirika la Nyumba la Taifa iliyopo Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kukagua miradi na kuhimiza utendaji kazi wenye kuleta tija kubwa.

Meneja wa NHC Mkoa wa Iringa Bi Esther Magese akiwasilisha taarifa ya Mkoa kwa Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Hamad Abdallah ambaye yupo Mkoani humo kukagua utendaji wa kazi na kuhimiza utendaji kazi wenye kuleta matokeo chanya.


Eneo la maduka ya biashara na nyumba za makazi lililopo Gangilonga katika Manispaa ya Iringa limetemebelewa na Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Hamad Abdallah ambaye yupo katika ziara ya kutembelea Mikoa ya Shirika la Nyumba la Taifa iliyopo Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kukagua miradi na kuhimiza utendaji kazi wenye kuleta tija kubwa.


Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Hamad Abdallah akikagua jengo la Ubia la Iringa Plaza ambapo amehimiza Shirika kufanya maamuzi ya kuhakikisha jengo hilo la ghorofa nne linaliletea Shirika tija iliyokusudiwa.


Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Hamad Abdallah akikagua jengo la Ubia la Iringa Plaza ambapo amehimiza Shirika kufanya maamuzi ya kuhakikisha jengo hilo la ghorofa nne linaliletea Shirika tija iliyokusudiwa.

. Asisitiza wafanyakazi kulinda mafanikio yaliyopatikana


. Ahimiza uadilifu na uzalendo ili kulipatia Shirika tija kubwa

. Aupongeza Mkoa wa Iringa kwa ubunifu

. Aahidi kuendelea kupigania maslahi bora kwa wafanyakazi

Na Mwandishi Wetu, Iringa

MKURUGENZI MKUU wa Shirika la Nyumba la Taifa Bw. Hamad Abdallah ameanza ziara ya kutembelea Mikoa ya NHC iliyopo Nyanda za Juu Kusini kama sehemu ya kukagua shughuli za Shirika, kuongea na wafanyakazi na kuhimiza utendaji wenye kuleta tija.

Akiwasili Mkoa wa Iringa na kukagua miradi mbalimbali iliyotekelezwa na Mkoa huo, Mkurugenzi Mkuu amefurahishwa na kuupongeza Mkoa huo kwa kuwa wabunifu katika kuliongezea Shirika mapato zaidi. 
 
" Nimefurahishwa sana na haya maduka ya biashara mliyobuni na kuyajenga katika viwanja vya Shirika ambavyo vilikaa miaka mingi bila kuliingizia Shirika mapato, hongereni sana na huu ni mfano wa kuigwa na kila Mkoa"

Akizungumza na wafanyakazi wa Mkoa huo, Mkurugenzi Mkuu amewashukuru kwa shukrani walizotoa kwake kutokana na nyongeza inayoridhisha ya mishahara na akaahidi kuendelea kupigania maslahi bora kwa wafanyakazi kama sehemu ya kuwaongezea ari ya kulitumikia Shirika kwa juhudi na maarifa.

"Mimi binafsi nafarijika kuona kiu yangu ya kufanikisha nyongeza ya maslahi ya wafanyakzi kwa kiwango ambacho serikalini huwezi kukipata imetimia, sasa mpira upo kwenu mkizalisha zaidi kwa faida ndani ya miezi sita sitasita kupiga hodi kwa Msajili wa Hazina kuwaombea fedha za likizo kwa utaratibu tuliokuwa nao zamani na kuwaombea kupewa posho ya nyumba"

Akasema kuwa siri pekee ya kuendelea kuongeza maslahi ya wafanyakazi ni kufanya kazi kwa bidii na kupata faida na kwamba safari hii hilo limewezekana baada ya Shirika kupata mapato yaliyofikia asilimia 135, hivyo akahimiza uadilifu na uchapaji kazi wenye tija ili tuendelee kulipana mishahara na maslahi bora kwa siku zijazo. Hivyo, akaupongeza Mkoa hio wa Iringa kwa kukusanya kodi kwa asilimia 105, kubuni miradi ya maduka ya kimkakati ya biashara, kufanya matengenezo ya nyumba na kupunguza kwa asilimia 74 ya madeni ya kodi ya nyumba.

"Huu ni mfano wa kuigwa, angalia sasa mapato ya haya maduka mliyojenga kwa muda mfupi na gharama nafuu za uwekezaji, yanazidi kwa mbali mapato ya jengo la ubia lenye ghorofa tano" 
 
Nawapongeza kwa kuwa wabunifu, mmeweza kuwa na mkakati bora wa kukusanya kodi kama timu moja kwa kuwapigia simu wadaiwa kwa mtindo wa kubadilishana majina ya wakati wa kupigia simu wadaiwa hao jambo linalowafanya waone sasa ni jambo la NHC yote"

"Mmewasiliana na taasisi za Serikali kuwafikia watumishi wao wanaodaiwa na mmekuwa na utaratibu wa vikao vya kila wiki kupanga mikakati ya kuliletea Shirika tija. Nimefurahishwa sana na Uongozi Shirikishi mlio nao. Chapeni kazi nasi Menejimenti tutaendelea kuwaunga mkono.

Akizungumzia uboreshaji wa taswira ya Shirika katika Mkoa huo, Mkurugenzi Mkuu ameahidi kujenga jengo kubwa la kisasa la biashara, Ofisi na makazi ambalo pia litawezesha Shirika Mkoani himo kuhamia katika jengo hilo ili kuwa na Ofisi za kisasa. 
 
Ameutaka Mkoa huo kutolitia tembo maji kwa kubweteka kutokana na mafanikio waliyoyapata, badala yake waendelee kubuni miradi yenye tija na akaahidi kuyafanyia kazi mapendekezo yao yenye lengo la kuongeza tija ya kibiashara ya Mkoa huo.

Wakati huo huo, amewapongeza wafanyakazi hao kwa kurejesha nyumba ya Shirika iliyokuwa inamilikiwa kinyemela bila Shirika kujuwa. Akawataka wafuatilie zaidi maeneo mengine yanayoashiria kuwa na majengo yanayoshabihiana na majengo ya zamani yaliyozoeleka kuwa ni ya NHC.

"Nilipokuwa napita katika mitaa na kukagua majengo yetu nimeona kama kuna majengo yanayofanana na ya NHC, huenda yanamilikiwa kinyemela, fuatilieni mjiridhishe ila msiingilie milki za watu kama hazituhusu, mjiridhishe tu"

Awali akitoa taarifa ya Mkoa huo kwa Mkurugenzi Mkuu, Meneja wa Shirika Mkoa wa Iringa Bi. Esther Magese alisema kuwa azma ya mkoa huo ni kufuta kabisa madeni sugu na kuongeza mapato kwa kuwa na uwekezaji wenye tija, na kwamba ujenzi wa maduka ya biashara walioufanya ni moja ya mikakati yao ya kuongeza mapato hayo.

Hivyo, ameuomba Uongozi wa Shirika kuutazama Mkoa wa Iringa kama moja ya mikoa yenye mahitaji makubwa ya nyumba za kupanga na ofisi kutokana na uwepo wa fursa za utalii na kilimo cha biashara. Akapendekeza Shirika kujenga majengo ya makazi, biashara na ofisi kwa kuwa tayari wana maombi mengi ya watu binafsi na taasisi zinazohitaji nyumba za aina hiyo.

Kwa niaba ya wafanyakazi ameushukuru Uongozi wa Shirika kwa kuwajali wafanyakazi na kuwangozea mishahara. " tumefurahi sana kwa nyongeza hii na tunakushukuru sana kwa uliotutendea, nasi hatutakuangusha katika uchapaji kazi, asante DG"

Katika hali ya kushangaza, wafanyakazi hao baada ya kufundishwa mada ya Huduma kwa Wateja na Meneja Habari na Uhusiano Bw. Muungano Saguya na kuwataka kupiga kura ya siri juu yakuridhika na huduma za NHC kwa wafanyakazi, wafanyakazi hao wengi wao waliridhika kwa asilimia 100 na wengine wachache walianzia asilimia 85 huku wakiomba nyongeza zaidi ya maslahi ikiwemo posho ya nyumba na likizo. 
 
Katika utafiti uliofanywa mwaka jana na Kampuni ya ABECC ya Chuo Kikuu Ardhi ilibainisha kuwa wafanyakazi wanaridhika na huduma za Shirika kwa asilimia 69.5 na utafiti kama huo uliofanywa na Synovate mwaka 2014 ulionyesha kuridhika kwa wafanyakazi kwa asilimia 76.

Mkurugenzi Mkuu leo anaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Mbeya na wiki ijayo ataifikia Mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi kukagua miradi inayotekelezwa katika Mikoa hiyo na kuzungumza na wafanyakazi.

Comments