Waziri wa Afya Atembelea Hospitali za Muhimbili Upanga na Mloganzila, Akisisitiza Kuendelea Kuboresha Ubora wa Huduma Nchini







Waziri wa Afya, Mheshimiwa Jenista Mhagama, amesisitiza dhamira ya Serikali katika kuboresha huduma za afya nchini, akieleza kuwa Serikali itazidi kusimamia ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi ili kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata huduma bora popote alipo na kwa wakati.

Kauli hii ilitolewa na Mheshimiwa Mhagama mapema leo, wakati alipofanya ziara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili - Mloganzila kwa lengo la kujionea jinsi huduma za uchunguzi na matibabu zinavyotolewa. Mheshimiwa Mhagama alilipongeza uongozi na watumishi wa Muhimbili kwa weledi na ubora wanaouonyesha katika kutoa huduma za afya kwa wananchi.

Waziri Mhagama alieleza kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa katika miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umewezesha hospitali hizi, hasa Muhimbili (Upanga na Mloganzila), kuwa na vifaa tiba vya kisasa, teknolojia ya hali ya juu, na wataalam waliohitimu. Hii imetusaidia kutoa huduma za ubingwa bobezi na kupunguza rufaa za kwenda nje ya nchi kwa matibabu.

“Sekta ya afya hapa Tanzania imeimarika zaidi kuliko kipindi chochote cha nyuma. Katika hospitali zetu za Taifa, hasa Muhimbili, tuna aina zaidi ya 35 za matibabu ya ubingwa bobezi, ikiwa ni pamoja na upandikizaji wa uloto, upandikizaji wa figo, na matibabu ya magonjwa ya moyo. Uwekezaji huu ni dhamira yetu ya kuhakikisha tunatoa huduma bora kwa Watanzania,” alisisitiza Mheshimiwa Mhagama.

Aidha, Mheshimiwa Mhagama aliongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa motisha na kuwajengea uwezo wataalam ili waweze kufuatilia mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayotokea duniani, kwa lengo la kuimarisha utoaji wa matibabu hapa nchini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Muhimbili, Dkt. Ellen Senkoro, alimuhakikishia Mheshimiwa Waziri kwamba bodi itashirikiana na menejimenti ya hospitali kuhakikisha kwamba maono ya Rais na maelekezo ya wizara yanatekelezwa, ili kila mtu anayepokea huduma Muhimbili apate huduma bora na zenye kiwango kinachokidhi matarajio yao.

Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Waziri aliambatana na viongozi wa Wizara ya Afya, akiwemo Naibu Katibu Mkuu Bw. Ismail Rumatila pamoja na baadhi ya wakurugenzi wa wizara hiyo.

Comments