Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali imetoa fedha takribani Sh. Trilioni sita tangu Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aingie madaraka kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo chini ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo wakati akitoa salam za Wizara kwenye mkutano wa hadhara wa kuhitimisha ziara ya siku sita ya Rais Samia mkoani Ruvuma uliofanyika kwenye uwanja wa Majimaji leo 28.09.2024.
Amesema “Mhe. Rais fedha ulizotoa zimeenda kila Mkoa, Halmashauri, Tarafa, Kata, Kijiji, Kitongoji na kila mtaa na zimegusa wanawake kwa wanaume, wazee, vijana, watoto na hata walemavu.”
“Hakuna kundi ambalo halijafikiwa na huduma zilizopelekwa kupitia fedha hizo ulizotoa, umegusa maisha ya watanzania, umegusa mioyo yao na umeboresha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi,”amesema.
Amefafanua miradi iliyotekelezwa kwa kipindi hicho kuwa ni Hospitali za Wilaya 129 mpya zimejengwa na hospitali Kongwe 50 zimekarabatiwa, Vituo vya Afya 367 vimejengwa, majengo ya kutoa huduma za dharura (EMD) 87 zimejengwa, Majengo ya kutoa huduma za Wagonjwa mahututi 28 yamejengwa, Mitambo ya kuzalisha hewa tiba ya Oksjen 21 imesimikwa, magari ya kubebea wagonjwa pamoja na usimamizi wa shughuli za Afya 523 yamenunuliwa.
“Kila Halmashauri nchini imepata gari la kubebea wagonjwa pamoja na gari la usimamizi wa shughuli za afya na hapa kwenye Mkoa wa Ruvuma wamepokea magari ya Wagonjwa kwa kila Halmashauri,”amesema
Aidha, amesema kwa upande wa elimu hadi sasa Shule mpya za Sekondari kwa Kata 458 zimejengwa, Shule za Msingi 665 zenye madarasa ya awali na vyumba vya madarasa 50,050 vimejengwa pamoja na nyumba za walimu 366 zimejengwa.
“Kwa upande wa TARURA umeongeza bajeti kutoka Sh.Bilioni 253 mpaka kufikia Sh.Trilioni 1.3, ongezeko hili ni zaidi ya asilimia 300 na hii ni kwa sababu unataka kuona barabara za vijijini zikifunguliwa na wananchi wanasafirisha bidhaa zao kwa urahisi.”
“ Mhe. Rais kupitia ongezeko hili umeweza kujenga barabara za lami maeneo ambao hayakudhaniwa kuwa na lami umepandisha hadhi barabara nyingi za vijijini na mijini na zaidi umeagiza tuongeze mtandao wa barabara za lami yenye urefu wa Kilometa 23 na kwa hapa Songea Manispaa tu barabara ya lami itajengwa yenye urefu wa Kilometa 12.
No comments:
Post a Comment