NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto
Biteko,akizungumza wakati wa uiznduzi wa jengo la Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) lililoenda sambamba na utiaji saini wa mikataba sita ya
utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi za
kupikia,hafla iliyofanyika leo Septemba 13,2024 jijini Dodoma.Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko (kulia) akifunua kitambaa kuashiria uzinduzi jengo la Wakala wa
Nishati Vijijini (REA)lililopo jijini Dodoma. Kushoto ni Mwenyekiti wa
Bodi ya REA, Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu. Wa pili kushoto ni
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi MrambaNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko akishuhudia Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Mhandisi Hassan Saidy, na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CPG)
Jeremia katungu wakionesha mkataba wa ushirikiano wa utekelezaji
wa Nishati Safi ya Kupikia mara baada kuusaini.SEHEMU ya washiriki wakimsikiliza Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko (hayupo pichani) ,akizungumza wakati
wa uiznduzi wa jengo la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) lililoenda
sambamba na utiaji saini wa mikataba sita ya utekelezaji wa mkakati wa
kitaifa wa matumizi ya nishati safi za kupikia,hafla iliyofanyika leo
Septemba 13,2024 jijini Dodoma.
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Dk. Doto Biteko,akishuhudia utiaji saini wa mikataba sita ya
utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia
kati ya REA na Jeshi la Magereza na Jeshi la kujenga Taifa (JKT),hafla
iliyofanyika leo Septemba 13,2024 jijini Dodoma.
NAIBU
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto Biteko amesema Serikali
inafanya kila jitihada kuhakikisha kunakuwa na unafuu katika
upatikanaji wa bidhaa za nishati safi ya kupikia ikiwemo mitungi ya
gesi ili kumwezesha kila mwananchi kutumia nishati iliyo safi na
salama.
Katika
kutekeleza jitihada hizo, Serikali imetoa ruzuku kwa mitungi ya gesi
zaidi ya 400,000 itakayouzwa kwa nusu gharama ya awali ambayo
inasambazwa katika mikoa yote Tanzania Bara huku zoezi hilo likiwa ni
endelevu.
Dkt.
Biteko amesema hayo tarehe 13 Septemba 2024 jijini Dodoma wakati wa
hafla ya Kusainiwa mikataba ya ushirikiano ya utekelezaji wa Nishati
Safi ya Kupikia yenye thamani ya shilingi bilioni 50.98 kati ya Wakala
wa Nishati Vijijini (REA) na taasisi sita ambazo ni Jeshi la Kujenga
Taifa (JKT) Jeshi la Magereza (TPS) na Wasambazaji wa Gesi ya kupikia,
hafla ambayo ilienda sambamba na uzinduzi wa jengo la REA.
“Namshukuru
Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake yanayowezesha Sekta ya
Nishati kuendeshwa kwa mafanikio ambayo yamepelekea leo hii tushuhudie
hatua ikizidi kupigwa katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya
Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kuokoa maisha ya watanzania na pia
kuiwezesha Wizara ya Nishati kutatua changamoto zinazojitokeza lengo
likiwa ni kutoa huduma iliyo bora kwa wananchi.” Amesema Dkt. Biteko
Kuhusu
mikataba hiyo ya Nishati Safi ya Kupikia, Dkt.Biteko ameiagiza REA na
wadau kuhakikisha kuwa matokeo yanaonekana tena kwa uharaka akieleza
kuwa “itakuwa aibu sana watanzania wanaona mikataba imesainiwa huku
kukiwa hakuna matokeo, tusione kawaida kwa ndugu zetu kupoteza maisha
kwa kutumia nishati isiyo safi, tuwaokoe kupitia miradi hii na tutumie
kila fursa inayojitokeza.”
Amesisitiza
kuwa, ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ni ya wote na inalenga kuokoa
maisha ya watanzania hivyo hivyo iwe ni kipaumbele cha watu wote.
Kuhusu
usambazaji wa nishati vijijini ikiwemo umeme, ameipongeza Bodi ya REA
kwa kusimamia ipasavyo miradi hiyo vijijini na kwa kuwahimiza
wakandarasi kukamilisha kazi kwa wakati.
Akizungumzia
jengo la REA alilolizindua, Dkt.Biteko amesema litawawezesha watumishi
kutoa huduma kwa wananchi na kuwapongeza REA kwa kujenga jengo hilo la
kisasa lenye ghorofa tano kwa gharama ya shilingi bilioni 9.8 kwa miezi
18 badala ya shilingi bilioni 13 zilizopangwa awali.
Pamoja
na kuipongeza REA kwa ujenzi wa jengo hilo la kisasa amewakumbusha
kuwa, uwepo wa jengo wa jengo hilo lazima uende sambamba na utoaji wa
huduma bora kwa wananchi.
“
Mimi naamini Jengo hili kweli ni muhimu lakini muhimu zaidi ni huduma
kutoka kwenu kwenda kwa wananchi, kama tunasema kwamba tuna jengo zuri
la ghorofa tano, halafu tukatoa huduma mbaya, jengo hili halitakuwa na
maana yoyote hivyo uzuri wake uonekane kwenye huduma kuanzia sehemu ya
mapokezi na wananchi watoke katika jengo hili wakiwa na furaha.”
Amesisitiza Dkt. Biteko
Katika
hatua nyingine, Dkt. Biteko ameagiza Watendaji wa Wizara ya Nishati
kuhakikisha kuwa majengo ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake yanafungwa
mfumo wa umeme jua ikiwa ni kuonesha kwa vitendo matumizi ya nishati
safi yenye gharama nafuu.
kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe.Daniel Sillo
amesema tukio hilo ni alama ya ushirikiano kati ya REA na Taasisi za
Jeshi ambapo amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake
za dhati katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, udhibiti wa
rasilimali za misitu na kutengeneza fursa za ajira kupitia Nishati Safi
ya Kupikia.
Amesema
kusainiwa kwa mikataba hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais, Dkt.
Samia na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya
Kupikia (2024-2034) kuwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 ziache
matumizi ya kuni na mkaa na kuanza kutumia vyanzo vya Nishati safi ya
Kupikia ikwemo gesi asilia, umeme, bayogesi na makaa ya mawe
yaliyoboreshwa.
Amesema
kwa sasa nishati inayotumika kupikia chakula cha Wafungwa na Mahabusu
ni kuni kwa asilimia 98 ambapo Jeshi hilo lilianza kutekeleza Mkakati
wa Nishati Safi ya Kupikia kwa kuanza kutumia nishati safi kupitia gesi
asilia na mkaa mbadala hivyo kusainiwa kwa mkataba huo kutawezesha
Jeshi la Magereza kutumia nishati safi ya kupikia kwenye magereza yake.
Amesema
kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani itahakikisha fedha zilizotengwa pamoja
vifaa kwenye programu hiyo zinasimamiwa ipasavyo ili lengo tarajiwa
lifikiwe na hii ikienda sambamba na utoaji wa mafunzo kwa watumishi wa
Jeshi ili waweze kuisimamia na kutunza miundombinu itakayofungwa.
Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ametoa pongezi kwa REA kwa
kukamilisha jengo kubwa la kisasa ambalo linaifaharisha Dodoma na pia
amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa sh.bilioni 214 kwa
ajili ya shughuli za umeme mijini na vijijini ambapo mkoani Dodoma
asilimia 92.2 ya vijiji vimefikiwa na umeme huku kazi hiyo usambazaji
umeme ikiendelea.
Pia
amempongeza Rais, kwa miradi ya Nishati Safi ya Kupikia kupitia
uhamasishaji wa nishati hiyo na kueleza kuwa kasi ya kutumia nishati
safi kwa wananchi inaongezeka.
Kwa
upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi
Mramba amesema kusainiwa kwa mikataba hiyo ni utekelezaji wa agizo la
Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alilolitoa wakati akizindua mjadala wa
kitaifa wa Nishati Safi ya kupikia na kutilia mkazo wakati akizindua
Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na kwamba Wizara
ya Nishati ina wajibu wa kutekeleza agizo hilo na ndio maana taasisi
yake ya REA imesaini mikataba husika
Amesema
Mikataba iliyosainiwa inahusisha masuala mbalimbali ikiwemo kufunga
mifumo ya nishati safi ya kupikia pamoja na usambazaji wa majiko na
mitungi ya gesi ipatayo laki nne ambayo inatolewa kwa bei ya ruzuku kwa
wananchi hasa maeneo ya vijijini.
Awali,
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan
Saidy alisema kuwa, Wakala huo kuhamia kwenye jengo lake kumewezesha
kuokoa shilingi milioni 650 zilizokuwa zikitumika kwa mwaka kulipia kodi
ya pango ambazo sasa zinaelekezwa kwenye maendeleo ya huduma
zinazotolewa.
Kuhusu
mikataba ya Nishati Safi ya Kupikia alisema kwa upande wa Jeshi la
Magereza, mikataba iliyosainiwa ina thamani ya shilingi bilioni 35.23
ambapo kati ya fedha hizo 75.5% ambayo ni sawa na shilingi bilioni 26.57
zitatolewa na REA na 24.6% sawa na shilingi bilioni 8.66 zitatolewa na
Jeshi hilo kwa mradi utakaotekelezwa kwa muda wa miaka mitatu katika
Magereza 129 ya Tanzania Bara.
Mkataba
wa Magereza unahusisha masuala mbalimbali ikiwemo ujenzi wa mifumo ya
bayogesi (gesi vunde) 126, usimikaji wa mifumo 64 ya gesi ya LPG,
usimikaji wa mfumo wa gesi asilia, usambazaji wa mitungi ya gesi (LPG)
ya kilo 15 ikiwa na jiko la sahani mbili ipatayo 15,920 kwa watumishi wa
Magereza na usambazaji wa tani 865 za mkaa mbadala unaotokana na makaa
ya mawe kutoka STAMICO.
Mhandisi
saidy alisema kwa upande wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mikataba
iliyosainiwa ina thamani ya shilingi bilioni 5.75 ambapo kati ya fedha
hizo asilimia 76 ambayo ni sawa na shilingi bilioni 4.37 itatolewa na
REA na huku asilimia 24 sawa na shilingi bilioni 1.39 itatolewa na JKT.
Amesema
fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi katika Kambi 22 za JKT kwa muda
wa miaka miwili itakayohusisha ujenzi wa mitambo 9 ya bayogesi, majiko
291 ya kutumia mkaa mbadala (makaa ya mawe na tungamotaka), ujenzi wa
mifumo 180 ya kupikia inayotumia LPG na sufuria zake, ununuzi wa tani
110 za mkaa unaotokana na makaa ya mawe, ununuzi wa mashine 60 za
kutengeneza mkaa mbadala na mafunzo kwa vijana wapatao 50,000.
Wadau
wengine waliosaini mikataba ya Nishati Safi ya Kupikia ni kampuni
zinazofanya biashara ya gesi ya mitungi ikiwemo Taifa Gas, Manjis, Oryx
pamoja na Lake Oil ambapo wanasambaza mitungi ya gesi ya kupikia ipatayo
452,445 kwa bei ya ruzuku katika mikoa yote ya Tanzania Bara.