Thursday, December 01, 2016

MENEJA WA TANROADS MKOA WA SHINYANGA AELEZEA UTEKELEZAJI WA MIRADI MKOANI KWAKE

   Meneja wa Mkoa wa TANROADS  Shinyanga (katikati) akipewa maelezo juu ya ujenzi wa Barabara ya Mwigumbi – Maswa (km 50.30) na Mhandisi Mshauri  wa Kampuni ya Kikandarasi ya KYONGDONG Engineering Co. Ltd  ndugu Kim Hyung Gyu
  Ndugu Kim Hyung Gyu – Mhandisi Mshauri  akitoa ufafanuzi juu ya utekelezaji wa mradi wa maendeleo ya kitaifa wa Mwigumbi – Maswa (km 50.30) kwa Meneja wa Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Augustino Wittonde Phillipo.
  Meneja wa Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Augustino Wittonde Phillipo akikagua culvert la dharura yanayo tumika wakati barabara inapokatika kutokana  mafuriko kulia ni Afisa Habari Mkuu wa TANROADS Bi. Aisha Malima
  Kazi za ujenzi katika barabara ya Mwigumbi – Maswa (km 50.30) zikiendelea

Meneja wa TANROADS mkoa wa Shinyanga Mhandisi Wittonde Philipo ameelezea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara mkoani mwake na kueleza kwamba maendeleo ya miradi mkoani   mwake ni mazuri.
Akiongea na Afisa habari wa TANROADS Bi. Aisha Malima, Mhandisi Phillipo alisema kuwa miradi miwili ipo katika hatua za kati na mwisho katika utekelezaji wake.

Miongoni mwa miradi iliyotembelewa na Afisa Habari huyo  na ujumbe wake ni barabara ya Mwigumbi – Maswa yenye kilometa  50.30 inayounganisha mkoa wa Shinyanga na Simiyu.Kwa upande wa mkoa wa Shinyanga ni kilometa 16 na kilometa 34 mkoa wa Simiyu. 

Mradi huu umeanza mwaka jana mwezi wa sita na matarajio ni kumaliza Aprili  mwaka ujao. Utekelezaji wa mradi huu ambapo kwa sasa ni asilimia 65 unasimamiwa na Kampuni ya Mkandarasi ya CHICO kutoka China pamoja na  Wahandisi Washauri wa Kampuni ya  KYONDONG Engineering Co. Ltd kutoka Korea ya Kusini, JV CORE  Consulting PLC ya Ethopia, LUPTA Consults Ltd ya Tanzania na ACE Consultants kwa gharama ya shilling billioni 61.461 na inafadhiliwa kwa asilimia mia moja na Serikali ya Tanzania.

Mhandisi Wittonde Phillipo alielezea changamoto kadha zilizojitokeza wakati wa ujenzi wa barabara hizo kuwa ni ukosefu wa maji kwa ajili ya kazi ya ujenzi. Aidha wakati wa masika mkandarasi aliweka jitihada ya kuchimba mabwawa kuhakikisha kazi haisimami kutokana na ukosefu wa maji.
Changamoto nyingine ilikuwa eneo la kujenga barabara ambapo  alitumia fursa kuwashukuru wananchi walio toa ushirikiano wa kutosha na walio vunja nyumba zao bila ya matatizo yeyote.

Mhandisi Phillipo alieleza kwamba barabara hii inaendelea vizuri na kwa sasa mkoa wa Shinyanga una miradi mingi  ambayo imekamilika kwa kiwango cha lami .

Ujumbe huo ulimaliza ziara yake kwa kutembelea mradi wa barabara ya mkoa ya Uhuru ambayo iko eneo la Lubaga inayojengwa kwa fedha za Serikali kwa asilimia mia moja. Barabara hii ya katikati ya mji itakuwa  na upana wa mita 6.5  na sehemu ya watembea kwa miguu na waendesha pikipiki ya miguu miwili na mitatu.

Barabara hii inajengwa na Mkandarasi mzawa JOTAN Engineering ikiwa ni mkakati mojawapo iliyowekwa kuhakikisha nao wakandarasi wazawa wanapewa nafasi katika miradi ya ujenzi wa barabara.

Afisa Habari huyo wa TANROADS alitoa wito kwa wananchi watunze barabara ambazo zinajengewa kwa pesa ya kodi za wananchi na kuomba madereva wahakikishe hawazidishi uzito katika magari kwa lengo la kulinda barabara ziweze kudumu kwa muda uliopangwa.

Alimaliza kwa kusema kwamba alama za barabarani pia zina umuhimu mkubwa na zinaitajika pia kulindwa ili kunusuru maisha ya watu na mali zao kwani zikikosekana zinaweza kusababisha ajali.

Afisa Habari huyo alimtembelea Mhandisi wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga katika ziara ya kikazi iliyolenga kupata habari za utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara mkoani humo.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...