Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Mhe. William Lukuvi amevifutia hatimiliki viwanja 15 vilivyokuwa vinamilikiwa na raia mmoja wa Uingereza ambapo serikali imevitaifisha viwanja hivyo vilivyopo katika mikoa ya kanda ya ziwa.
Viwanja hivyo vilivyokuwa vinamilikiwa na Mfanyabiashara maarufu jijini hapa, Hermant Patel, mwenye uraia wa Tanzania na Uingereza kitendo ambacho ni kinyume na taratibu na sheria za nchini zinazozuia raia wa kigeni kumiliki ardhi.
Aidha, Mhe. Lukuvi amesema anayeruhusiwa kumiliki ardhi nchini ni raia wa Tanzania pekee na kuongeza kwamba kwa watanzania waishio nje ya nchi na kuukana uraia wao nao hawataruhusiwa kumiliki ardhi bali watapewa ardhi kama ilivyo kwa wawekezaji kutoka mataifa mengine.
Mhe. William Lukuvi amesema mtu akishaukana uraia wa Tanzania hana haki tena kama raia wa Tanzania, hivyo ataruhusiwa kumiliki ardhi kama mwekezaji tu na siyo kama raia wa Tanzania. Lukuvi amesisitiza kuwa ardhi itabaki kuwa ya Watanzania tu na ameagiza mamlaka zota kutawasaka wale wote ambao wanamiliki ardhi kinyume na sheria za nchi.
Uamuzi wa kufuta hatimiliki hizo ulitolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, William Lukuvi wakati akizungumza na wanahabari juu ya hatua hiyo ya Serikali ya kuvifuta hati hizo jijini Mwanza.
Lukuvi alisema kuwa awali Serikali ilikuwa ikifahamu mfanyabiashara huyo anahatimiliki ya viwanja vitano lakini baada ya uchunguzi uliohusisha Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mwanza wamebaini raia huyo anamiliki viwanja 15.
Alisema kuwa kitendo cha mfanyabiashara huyo kumiliki, viwanja 15 katika mikoa ya kanda ya ziwa kwa njia ya udanganyifu kumeonesha ni namna gani raia wa kigeni wasivyokuwa waaminifu na kuwakanya kuacha mchezo huo.
“Viwanja hivi tumevitaifisha na sasa vimerudi chini ya Serikali na baada ya hapo vitapigwa mnada, hatutakubali kuona watu ambao sio wazawa wakilimiki ardhi kiasi hicho.
“Huyu Patel (Hermant Patel) alikuwa na paspoti (hati za kusafiria) mbili za Tanzania na Kenya hiyo imeonesha ni namna gani alivyotapeli na wale wote wenye paspoti mbili wakae chonjo,” alisema Lukuvi.
Lukuvi ambaye pia ni Mbunge wa Isimani mkoani Iringa, alisema kuwa wizara ya ardhi ni miongoni mwa wizara zinazotumika kupitisha utakatishaji wa fedha haramu huku akidai raia wengi wa kigeni wanaonunua ardhi hutakatisha fedha chafu.
Hata hivyo, alisema kuwa baadhi ya watumishi katika wizara yake wameonekana kutokuwa makini katika usimamizi mzuri wa utoaji wa hati za umiriki ardhi kwa raia wa kigeni kitendo ambacho alikikemea na kuwataka kubadilika.
Baadhi ya viwanja vilivyofutiwa hatimiliki na kutaifishwa na Serikali ni pamoja na kiwanja namba 98 kitalu ‘ F’ nyakato Mwanza, kiwanja namba 45 Mkuyuni Mwanza, Viwanja namba 539 na 560 kitalu ‘A’ Magongo Geita.
Vingine ni kiwanja namba 113 kitalu ‘A’ Nyamhongoro Mwanza, kiwanja namba 798 Magongo Geita, kiwanja namba 529 Magogo – Geita, viwanja namba 531 na 532 Bombambili Geita na viwanja namba 533 na 534 kilichopo Geita.
Viwanja vingine ni kiwanja namba 332 Kilichopo Bwiru Ilemela Mwanza, namba 330 kitalu ‘A’ Bwiru Ilemela Mwanza, namba 115 Nyamhongoro Mwanza, kiwanja namba 3 kitalu ‘C’ kilichopo Lamadi Busega mkoani Simiyu na kiwanja namba 1 na 2 vilivyopo Lamadi – Busega mkoani.
Mhe. Lukuvi Ameyasema hayo leo katika ofisi ya Ardhi ya Kanda ya Ziwa iliyopo mkoani Mwanza.
No comments:
Post a Comment