Monday, July 12, 2010
Mgombea Mwenza wa CCM ni Dk Gharib Bilal
BAADA ya kuangushwa mara tatu katika mbio za kuwania urais wa Zanzibar, nyota na nguvu za kisiasa za Dk Mohamed Gharib Bilal zilizidi kujidhirisha baada ya kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete kwenye mbio za urais wa Muungano katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 31.
Uteuzi huo wa Dk Bilal, ambao ulitangazwa kwenye mkutano mkuu wa CCM uliofanyika Kizota mjini Dodoma, umefanywa katika kipindi ambacho joto la kisiasa ndani ya CCM lilikuwa limepanda baada ya halmashauri kuu ya chama hicho kumtupa msomi huo kwa mara ya tatu kwenye mbio za urais.
"La mwisho kabla ya mwisho," alisema Kikwete na kuacha muda kidogo akisikiliza majibu yan wanachama ambao walipiga kelele kutaka kutangaziwa jina la mgombea mwenza atangazwe baada ya kusubiri kwa muda mrefu.
"La mwisho kabla ya mwisho, nimemteua Dk Bilal kuwa mgombea mwenza."
Mara baada ya tamko hilo ukumbi mzima ulilipuka kelele za nderemo na vifijo, miruzi na maturumbeta mithili ya mavuvuzela huku Bilal akikumbatiwa na watu tofauti wakati akianza kuelekea kwenye meza kuu.
Wakati Bilal akipongezwa, kikundi cha muziki cha CCM, ToT Plus kilianza kutumbuiza huku Rais Kikwete akicheza muziki na uso wake ukiwa umepambwa kwa tabasamu kuonyesha kufurahishwa na kelele za wajumbe ambazo zilionyesha kukubali uteuzi huo.
Bilal alikwenda moja kwa moja kwenye meza kuu na kuwashika mikono viongozi wote, akimkumbatia Rais Kikwete na baadaye kwenda kwenye jukwaa lililokuwa likitumiwa kutoa hotuba kwa ajili ya kutoa shukrani. Hata hivyo, wajumbe waliendelea kujimwaga ukumbini kushangilia wakicheza muziki wa ToT.
Lakini wakati Dk Bilal akiendelea kusubiri wajumbe watulie ili azungumze, afisa mmoja alimwendea na kumnongeza jambo na ndipo waziri kiongozi huyo wa zamani wa Zanzibar alipoondoka na kurudi kwenye kiti chake.
Kabla ya kumtangaza Dk Bilal, Kikwete aliomba mkutano uende mapumziko kwa dakika 15 ili akutane na wajumbe wa kamati kuu, lakini kikao hicho kilichukua takriban nusu saa na aliporejea alianza na hotuba ndefu ya kueleza mafanikio na matatizo ambayo serikali ya awamu ya nne ilikutana nayo tangu mwaka 2006.
Awali majina mbalimbali yalikuwa yakihusishwa na nafasi hiyo, ikiwa ni pamoja na Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha, waziri wa zamani wa fedha, Zakia Meghji, na Waziri wa Nchi, Mohamad Seif Khatibu ambaye ni Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais -Muungano kabla ya kitendawili hicho kuteguliwa saa 3:30 usiku. Imeandikwa na Exuper Kachenje, Dodoma na Ramadhan Semtawa, Dar. SOURCE: MWANANCHI.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA
Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...
-
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu na timu ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa akiwa katika ...
-
NATIONAL EXAMINATIONS COUNCIL OF TANZANIA PSLE-2014 EXAMINATION RESULTS ARUSHA DAR ES SALAAM DODOMA IRINGA KAGERA KIGOMA ...
-
Adam Malima James Wanyancha Hamis Kagasheki RAIS Jakaya Kikwete ameteua Baraza la Mawaziri, huku likiwa na sura na damu mchanganyiko. Bar...
No comments:
Post a Comment