Thursday, July 08, 2010
Kabudi: Propaganda inatumika EAC
Mkuu wa Kitivo cha Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mlimani(UDSM) Profesa Palamagamba Kabudi (katikati)akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam jana, wakati wa mkutano wa kujadili nafasi ya vyombo vya habari katika soko la pamoja, kushoto ni kaimu mwenyekiti wa MCT na Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi Theophil Makunga na kulia ni Katibu wa Jukwaa la Wahariri nchini, Neville Meena.Picha na Venance Nestory.
*************************************************
MSIMAMO wa Tanzania katika kuhakikisha inazilinda fursa mbalimbali zilizopo nchini ikiwemo ardhi, zinabaki kuwa chini ya miliki ya Watanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) umesababisha kuhujumiwa pamoja na kuenezwa propaganda chafu.
Propaganda hizo zinafuatia msimamo wa Tanzania kutokuwa tayari kufungua milango kwa nchi EAC kuingia nchini na kumiliki ardhi, kupewa ukazi wa kudumu pamoja na vitambulisho vya uraia kutumika kama pasipoti za kuingilia katika nchi hizo.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na mjumbe wa Tanzania katika Kamati Maalumu ya majadiliano ya EAC, Profesa Palamagamba Kabudi katika mkutano wake na Jukwaa la Wahariri nchini.
Mkutano huo ulikuwa na lengo la kujua nafasi ya vyombo vya habari katika Soko la Pamoja la Afrika Mashariki lililoanza Julai Mosi mwaka huu.
Profesa Kabudi alisema baadhi ya nchi ndani ya jumuiya hiyo zinaisema vibaya Tanzania juu ya mambo zaidi ya saba ambayo hayamo kwenye jumuiya hiyo.
Profesa Kabudi ambaye pia ni Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alifafanua kuwa katika suala la ardhi walikataa baada ya kuzingatia matokeo ya tafiti ambazo zilionyesha idadi kubwa ya Watanzania hawataki suala hilo kuingizwa katika ushirikiano.
Kuhusu suala la vitambulisho vya uraia kutumika kama pasi za kusafiria, alisema uamuzi huo ulifikiwa ili kulinda usalama wa nchi kutokana na Tanzania kuwa ndio nchi pekee barani Afrika kupakana na nchi kumi.
Kuhusu ukazi wa kudumu, Profesa Kabudi alisema kulingana na mazingira pamoja na jinsi fursa za ukazi zilivyo katika nchi za EAC, ni vigumu kwa Watanzania kwenda kuomba ukazi katika nchi hizo na kwamba wananchi wengi katika nchi hizo wangekimbilia nchini.
Hata hivyo, Profesa Kabudi alisema baadhi ya mambo ambayo Tanzania imefungua milango yake ni utoaji wa ajira, ujenzi wa hoteli za ghorofa pamoja na ujenzi wa shule.
Alisema uingizwaji wa masuala hayo katika Soko la Pamoja limezingatia maslahi ya taifa na hivyo Tanzania haipaswi kulaumiwa kwa lolote kwa kuwa hata katika mkataba wa EAC ibara namba 75 umeelekeza masuala mbalimbali yasiharakishwe kuingizwa katika ushirikiano.
Kuhusu kiwango cha elimu inayotolewa Tanzania alisema ni bora kuliko ya nchi nyingine isipokuwa wengi huishusha kwa kuithaminisha kwa lugha ya Kiingereza.
Alifafanua kuwa pamoja na kufunguliwa kwa itifaki ya soko hilo, Watanzania na nchi wanachama wasitegemee masuala yote yaliyokubaliwa kwenye soko hilo yatatekelezwa mara moja na kwamba mchakato wa utekelezaji wake utakwenda taratibu.
Alisema kila nchi inapofanya maamuzi juu ya suala lolote kwanza inazingatia maslahi yake na si vingenevyo.Imeandikwa na Sadick Mtulya na Hussein Kauli: SOURCE MWANANCHI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA
Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...
-
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu na timu ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa akiwa katika ...
-
NATIONAL EXAMINATIONS COUNCIL OF TANZANIA PSLE-2014 EXAMINATION RESULTS ARUSHA DAR ES SALAAM DODOMA IRINGA KAGERA KIGOMA ...
-
Adam Malima James Wanyancha Hamis Kagasheki RAIS Jakaya Kikwete ameteua Baraza la Mawaziri, huku likiwa na sura na damu mchanganyiko. Bar...
No comments:
Post a Comment