Monday, June 08, 2009

Mahakama: Mahalu hana kinga kushitakiwa



MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imetupilia mbali maombi ya balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na mwenzake kutaka kupitiwa upya kwa mwenendo wa kesi yao ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh2 bilioni.

Jaji Juxon Mlay alisema jana kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ina mamlaka zote kisheria kuendesha kesi hivyo akaamuru kesi hiyo iendelee kusikilizwa katika mahakama hiyo.

Awali katika maombo ya upande wa utetezi ulidai kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ua kusikiliza kesi hiyo kwa kuwa washtakiwa wanakinga ya kibalozi na kwamba makosa hayo yalifanyika nje ya Tanzania.

Alisema hoja kuhusu ushahidi wa mwisho uliochukuliwa kwa njia ya video hawezi kuizungumzia kwa sabababu suala hilo tayari lilishatolewa uamuzi na Mahakama ya Kisutu.

Pia alisema sheria za Tanzania zinaweza kuingilia nchi yeyote na kwa mtu yeyote mwenye kinga ambaye atakuwa ametenda makosa nje ya nchi isipokuwa rais.

“Mwenye kinga ya moja kwa moja ni rais tu na suala hilo liko kwenye katiba kwa washitakiwa hawa kinga ingeweza kuwasaidia wakiwa kule Italia, lakini si hapa kwetu,” alisema Jaji Mlay.

Hata hivyo akizungumza nje ya mahakama mara baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, mmoja wa mawakili wa upande wa utetezi, Bobu Makani alisema watakata rufaa kwasababu hawajaridhika na uamuzi huo.

Mahalu na aliyekuwa ofisa Utawala wa ubalozi wa Tanzania nchini Italia, Grace Martin wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia hasara serikali ya zaidi ya Sh2 bilioni.

Mei 4, mwaka huu washitakiwa hao walitakiwa waanze kujitetea, lakini mawakili wao waliwasilisha Mahakama Kuu maombi ya kupitiwa upya kwa mwenendo wa kesi yao.

Katika maombi yao, upande wa utetezi unadai kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo vinginevyo kiwepo kibali cha Jaji Mkuu. Imeandikwa na Nora Damian wa Mwananchi.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...