Tuesday, October 30, 2007

Gongo yamuua akishangilia ushindi wa CCM

Na Abdallah Nsabi wa Mwananchi

FURAHA ya ushindi wa Chama cha Mapinduzi CCM kupata ushindi wa Udiwani imemtokea puani mkazi wa kata ya Nguliguli Wilayani Maswa Lonjini Petro (54) baada ya kunywa lita tatu za pombe aina ya gongo na kufariki dunia.

Tukio hilo lilitokea juzi katika kata hiyo baada ya kutangazwa matokeo ya ushindi wa chama hicho ndipo Petro alipokwenda nyumbani kwa Gumba Mboje na kuangiza lita tatu za gongo ili anywe afurahie ushindi huo ambao alikuwa anausubiri kwa hamu na kukutwa na mauti.

Chanzo cha habari kutoka katika eneo hilo kilisema kuwa Petro aliwekeana ahadi na mtu mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana kuwa iwapo chama cha CCM kingeshinda wangenunuliana pombe aina ya gongo na kunywa mpaka asubuhi.

Pia ilieleza kuwa Mara baada ya ushindi wa chama cha Mapinduzi CCM, marehemu aliamua kujikita katika moja ya nyumba ambayo wanafanya biashara hiyo na kisha kuanza kunywa pombe hiyo haramu hadi kukutwa na umauti papo papo.

Habari hizo zinaeleza kuwa marehemu ambaye enzi za uhai wake alikuwa kada wa chama hicho siku hiyo alionekana kuwa na furaha ya ushindi mara baada ya chama chake kutangazwa kushinda ndipo alipoamua kwenda kufakamia kinywaji hicho kwa majigambo kuwa amefurahi kushinda kwa mgombea wao.

Wakazi wa kata hiyo mara baada ya kumwona mwenzao amezidiwa kwa kinywaji hicho kutokana na kuanguka chini kwa kuzimia walianza kumwagia maji ya baridi huku wakimpepea lakini baada ya muda mfupi aliaga dunia.

Ilielezwa kuwa marehemu Petro alikuwa na kawaida ya kunywa pombe, lakini akuwahi kulewa sana kama ilivyotokea siku hiyo ambayo alikuwa akisherehekea ushindi wa chama chake hicho alichokuwa akikiunga mkono pamoja na kuwa na uanachama wa muda mrefu.

Mbunge wa jimbo la Maswa John Shibuda alithibitisha kutokea kwa kifo hicho cha mwanachama wa CCM na kuongeza kuwa hali hiyo ilimtokea wakati akishangilia ushindi wa mgombea wa CCM.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...