Kiongozi wa upinzani Micheal Sata ametangazwa kuwa rais mpya wa Zambia mapema hii leo baada ya uchaguzi uliokumbwa na vurugu zilizosababisha vifo vya watu wawili.
Tume ya taifa ya uchaguzi nchini humo ilisema Sata alishinda asilimia 43 ya kura dhidi ya asilimia 36 za rais anayeondoka Rupiah Banda licha ya kuwa vituo 7 kati ya 150 vya upigaji kura nchini humo vilikuwa bado vinaendelea kuhesabu kura hizo.
Tume hiyo ya uchaguzi ilisema kuwa idadi ya wapiga kura katika maeneo hayo ni ndogo ikilinganishwa na kura laki moja elfu 88 zilizo watofautisha wagombea hao wawili. Wagombea wengine 8 waligawanya kura zilizosalia.
Jaji mkuu Ernest Sakala alimtangaza Micheal Chilufya Sata kuwa rais aliyechaguliwa wa jamhuri ya Zambia.
Punde baada ya kutolewa tangazo hilo muda mfupi baada ya saa sita usiku kuamkia leo, wafuasi wa Sata walimiminika barabarani katika mji wa Lusaka wakisherehekea huku wakipiga honi za magari.
Polisi ya kupambana na fujo ilikuwepo ikitazama wafuasi hao wakisherehekea.
Ilisema kuwa watu wawili waliuawa hapo jana katika vurugu zilizozuka baada ya wafuasi wa Sata kulalamikia utaratibu na udanganyifu katika zoezi la kuhesabu kura hizo.
Waangalizi wanasema hawajapata ushahidi wa kuthibitisha tuhuma hizo za udanganyifu huku waangalizi wa Umoja wa Ulaya wamekilaumu chama cha Banda MMD, kwa kutumia vibaya rasilimali za serikali, zikiwemo vyombo vya habari na magari wakati wa kampeni.
Hii ilikuwa ni mara ya nne kwa Sata kugombea wadhifa wa rais na ushindi wake unakifanya chama chake cha Patriotic Front kuwa chama cha tatu pekee kuingia uongozini tangu nchi hiyo kujinyakulia uhuru kutoka kwa Uingereza mnamo mwaka 1964.
Chama cha Banda ambacho Sata alikuwa mwanachama hadi mwaka 2001 kufuatia mzozo wa uongozi, umekuwa uongozini kwa miongo miwili.
Licha ya kuwa kiongozi huyo mpya ni mwenye umri wa miaka 74, mvuto wake ulikuwa zaidi kwa vijana nchini humo na watu wasiokuwa na ajira, wanaoona kuwa wametengwa kutoka biashara ya uchimbaji madini ya shaba nchini humo iliyoufanya uchumi wa nchi hiyo kuwa mojawapo ya unaofanya kazi vizuri Afrika.Biashara hiyo imesaidia kuundwa nafasi laki moja za ajira nchini Zambia na serikali imejenga madaraja, viwanja vya ndege hospitali kutoka fedha zinazopatikana kwa uchimbaji madini ya shaba.
Sata alikuwa gavana wa jimbo na waziri bungeni, alishindwa kwenye uchaguzi mnamo mwaka 2001 na pia mwaka 2006 kwa Levy Mwanawasa wa chama hicho cha MMD. Na baadaye mwaka 2008 wakati Mwanawasa alipofariki kutokana na kiharusi, Sata alishindwa na Banda ambaye aliyekuwa makamu wa rais wa Mwanawasa, kwa tofauti ndogo ya kura kwenye uchaguzi maalum uliofanyika.