SHULE za sekondari za serikali zimeng'ara katika matokeo ya kidato cha sita baada ya wanafunzi wake tisa kuwa miongoni mwa wanafunzi kumi bora kitaifa.
Lakini shule hizo za serikali hazikuweza kufua dafu kwa upande wa wasichana baada ya shule binafsi kutoa wanafunzi nane kati ya kumi bora waliofanya vizuri kwenye mtihani huo wa kumaliza elimu ya juu ya sekondari.
Wanafunzi wote walioshika nafasi kumi za kwanza ni wavulana. Wanafunzi hao ni Japhet John wa Shule ya Sekondari ya Ilboru, Manyanda Chitimbo (Kibaha, Pwani), Hassan Rajab (Minaki, Pwani), Abdulah Taher, Stinin Elias, Paul Nolasco na Ephraim Swilla wote kutoka Mzumbe, Morogoro.
Wengine ni Alexander Marwa na Benedicto Nyato kutoka Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Tabora, wakati Samuel Killewo wa Shule ya Sekondari ya Feza Boys ndiye mwanafunzi pekee kutoka shule binafsi aliyeingia kumi bora.
Kwa upande wa shule za wasichana, Jacqueline Seni wa Shule ya Sekondari ya Marian Girls iliyo Bagamoyo mkoani Pwani ndiye aliyeongoza akiwa na wenzake Khadija Mahanga, Esther Mlingwa, Perpetua Lawi na Lilian Kakoko, wakati Gerida John na Subira Omary wanatoka Shule ya Sekondari Dakawa.
Wasichana wengine waliofanya vizuri ni Elaine Kinoti kutoka Ashira, Kilimanjaro, Ruth Pendaeli kutoka Shule ya Sekondari ya Morogoro na Cecilia Ngaiza kutoka St Joseph Ngarenaro, Arusha Cecilia.
Shule za Marian Girls, Mzumbe, Kibaha, Tabora Boys, Ilboru, Malangali, Kifungilo, Tukuyu, Feza Boys na Uru Seminary zimeingia katika kumi bora wakati shule ya High-View International, Fidel Castro, Sunni Madressa, Neema Trust, Mtwara Technical, Muheza, Tarakea, Uweleni, Arusha Mordern na Maswa Girls zimekuwa shule kumi zilizoshika mkia.
Jumla ya watahiniwa 55,764, ambao ni asilimia 88.86 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani huo mwaka huu, wamefaulu na kati ya hao wasichana waliofaulu ni 21,821 (sawa na asilimia 90.39) ya waliofanya mtihani na wavulana waliofaulu ni 33,943 (sawa na asilimia 87.90 ya wavulana waliofanya mtihani).
Kwa kulinganisha na mwaka jana wakati waliofaulu walikuwa wanafunzi 45,217 (sawa na asilimia 89.64), idadi ya watahiniwa waliofaulu imeongezeka kwa wanafunzi 10,048, hata hivyo asilimia ya ufaulu imepungua kidogo kwa asilimia 0.78 mwaka huu.
Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam, katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani(Necta), Dk Joyce Ndalichako alisema watahiniwa wa shule waliofaulu ni 45,217 sawa na asilimia 93.76 ya waliofanya mtihani; wasichana waliofaulu ni 17,905 sawa na asilimia 94.07 na wavulana ni 27,320 sawa na asilimia 93.56. Imeandikwa na Boniface Meena. SOURCE: Mwananchi.
Comments