Monday, November 02, 2009

Mbunge Ng'itu afariki dunia


BUNGE la Jamhuri ya Muungano limempoteza mbunge wake wa tisa tangu liingie rasmi mwaka 2005 baada ya Sigifrid Ng’itu, 55, wa Jimbo la Ruangwa mkoani Lindi kufariki dunia juzi usiku akiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa.

Kifo cha mbunge huyo, ambaye alikuwa amelazwa tangu Septemba 14 kwenye Kitengo cha Mifupa (Moi), kililifanya Bunge lilazimike kuahirisha kikao chake cha tano cha mkutano wa 17 hadi leo.

Tangu kuanza kwa Bunge la tisa la Jamhuri ya Muungano, jumla ya wabunge tisa wamekwishapoteza maisha ambao ni pamoja na Salome Mbatia (Viti Maalum, CCM), Amina Chifupa (Viti Maalum, CCM), Chacha Wangwe (Tarime, Chadema), Benedict Losulutya (Kiteto, CCM), na Juma Jamalidini Akukweti (Tunduru, CCM).

Wengine ni Richard Nyaulawa (Mbeya Vijijini, CCM), Faustin Kabuzi Lwilomba (Busanda, CCM) na Phares Kabuye (Biharamulo Magharibi, TLP), ambaye alifariki kwa ajali ya gari wakati akiwa amekata rufaa ya kupinga hukumu iliyobatilisha ubunge wake.

Lakini wakati Bunge likipoteza mtu wa tisa, katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa, alitumia msiba huo kuipigia debe CCM ili ishinde katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Akizungumza na waandishi wa habari katika lango kuu la Bunge, Makamba alisema mbunge huyo alikuwa ni amana kwa CCM, wananchi wa Ruangwa na Tanzania kwa ujumla na hivyo atakumbukwa daima.

“Pengo la jino la dhahabu huzibwa kwa dhahabu hivyo ninaamini wananchi wa jimbo lake hawatafanya makosa katika uchaguzi mkuu wa 2010 na watakichagua Chama Cha Mapinduzi,” alisema Makamba.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...